Kuna mito duniani ambayo hukumbukwa kwa kuwa chanzo cha maji na Kuna mito mingine hujulikana kwa kuwa mpaka wa nchi
Miongoni mwa mito adimu duniani inayobeba hadhi ya kipekee kama chemchemi ya maisha, historia, utalii na urithi wa taifa ni Mto Ruvuma,ambao unapuliza pumzi ya uhai kwa mikoa ya Ruvuma na Mtwara na kuwa chombo cha amani kwa nchi jirani ya Msumbiji.
Ni mto uliobeba kila aina ya hadithi: uzuri wa asili, mandhari ya kupendeza, fukwe za kuvutia, wanyama pori, maporomoko ya kusisimua, visiwa vya asili, na hata hadithi za vita ya ukombozi wa Afrika ya Kusini.
Mto unaobeba Mkoa mzima wa Ruvuma
Kwa mujibu wa Deborah Mwakanosya, Mratibu wa Utalii Kanda ya Kusini, Mto Ruvuma ni zaidi ya mto ni uti wa mgongo wa Mkoa wa Ruvuma kwa sababu Ndiyo mto pekee unaopita katika wilaya zote tano za mkoa wa Ruvuma ambazo ni Songea, Mbinga, Nyasa, Namtumbo na Tunduru.
Huo ndio mto mrefu kuliko yote Afrika Mashariki, ukiwa na urefu wa kilometa zaidi ya 800, ukianzia katika milima ya Matogoro Manispaa ya Songea kwenye kisima kidogo chenye mfereji mwembamba na kusafiri hadi Bahari ya Hindi.
“Kisima hicho kipo juu ya meta 1,500 kutoka usawa wa bahari, lakini kinapozalisha maji hayo ya mwanzo ya Mto Ruvuma, hayawezi kufananishwa na kazi kubwa yanayokwenda kufanya mbele,” anasema Mwakanosya kwa msisimko wa kipekee.
Maajabu ya asili yaliyosheheni fukwe na maporomoko
Katika wilaya ya Tunduru, Mto Ruvuma unapita ndani ya Hifadhi ya Taifa ya mazingira asilia ya Mwambesi, ambapo fukwe za kuvutia na visiwa vya asili huonekana kama mchoro wa msanii mahiri.
Katika eneo hilo, watalii huogelea, hupiga picha, huendesha mitumbwi na kushuhudia wanyama wa kila aina kuanzia tembo na simba, hadi mamba na samaki wa ajabu.
Ndani ya hifadhi hiyo hiyo, yapo maporomoko ya ajabu ya maji yanayojulikana kama Maporomoko ya Sunda ambako huonekana ndege mdogo zaidi duniani, anayeitwa pantiole, anayekula samaki akiwa hai huku akiogelea ndani ya mto.
Nguvu ya maji inayozalisha umeme na ajira
Safari ya Mto Ruvuma haikomi kwenye mandhari bali Katika eneo la Tulila wilayani Mbinga, maji ya mto huo yamegeuzwa kuwa chanzo cha nishati safi ya umeme kupitia mradi wa umeme wa maji unaoendeshwa na watawa wa Kanisa Katoliki. Hapo, megawati tano huzalishwa na kulisha vijiji vinavyozunguka.
Aidha, katika wilaya ya Songea, mto Ruvuma unapita katika shamba kubwa la kahawa la AVIV lenye ukubwa wa hekta 2,000, ambapo hekta 1,000 zimetumika kwa uzalishaji wa kahawa,linatoa ajira za kudumu 1,400 na ajira za msimu 5,000.
ambako zaidi ya wafanyakazi 3,000 wamepata ajira kupitia kilimo cha umwagiliaji kwa kutumia njia ya matone ya Mto Ruvuma.
Utalii wa kihistoria, vita ya majimaji na uhuru wa Afrika
Si vivutio vya asili pekee vinavyohusiana na Mto Ruvuma.
Historia ya Tanzania na ukombozi wa Afrika Kusini inalindwa pia na mto huu. Maji ya Mto Ruvuma yalitumika katika Vita ya Majimaji dhidi ya ukoloni wa Kijerumani (1905–1907).
Eneo la Sunda lilibeba mapambano ya vita ya Golira War – mapigano ya msituni yaliyosaidia kuikomboa Msumbiji.
Kwa mujibu wa Mwakanosya, eneo la Negomano nchini Msumbiji, ambapo mito ya Ruvuma na Rujenda hukutana, lilikuwa ngome ya wanamapambano dhidi ya ukoloni wa Kireno.
Mpaka wa Tanzania na Msumbiji ni Mto Ruvuma, na eneo hilo pia linaelekeza kwenye Hifadhi ya Taifa ya Niassa ya pili kwa ukubwa nchini Msumbiji.
Daraja la Umoja: Mlango wa kuunganisha mataifa
Katika Wilaya ya Nanyumbu,mkoani Mtwara mto Ruvuma umepambwa kwa daraja la kipekee lenye urefu wa meta zaidi ya 700 Daraja la Umoja, linalounganisha Tanzania na Msumbiji kupitia Kituo cha Uhamiaji cha Mtambaswala.
Kwa mujibu wa Afisa Mahusiano wa Kituo hicho Mwamba Lihami, eneo la darajani hilo lina mvuto wa kipekee kielimu na kijiografia ni makutano ya mito miwili, Ruvuma na Rujenda, na majimbo mawili ya Msumbiji ambayo ni Delgado na Niassa.
Ruvuma hadi Baharini – safari ya maji yasiyokoma
Mto Ruvuma unaendelea kupitia wilaya ya Masasi hadi eneo la Msimbati, Mtwara mahali ambapo maji yake yanamwaga kwenye Bahari ya Hindi.
Hapo ndipo Hifadhi ya Bahari ya Ghuba ya Mnazi na Maingilio ya Mto Ruvuma ilipoanzishwa mwaka 2000, ikiwa na eneo la zaidi ya kilometa 650 za mraba.
Mhifadhi wa hifadhi hiyo, Devis Orio, anaeleza kuwa eneo hilo lina hazina kubwa ya viumbe wa baharini na nchi kavu kuanzia samaki wa kipekee hadi viumbe wa matumbawe.
Mto wa maisha na matumaini kwa vizazi vijavyo
Mto Ruvuma pia ni chanzo cha miradi ya maji inayowanufaisha maelfu ya wakazi wa vijiji vya wilaya za Masasi na Nanyumbu.
Mradi mkubwa wa maji kutoka Mto Ruvuma umeazishwa katika vijiji vya Masuguru na Chipingo.
Mto Ruvuma ni mzizi wa maendeleo, kitovu cha utalii, mlango wa historia ya ukombozi, na kielelezo cha uzuri usio na kifani wa kusini mwa Tanzania.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: KERO PIGA 0800110174
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.