Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Kanali Ahmed Abbas Ahmed, amesema Serikali inatambua mchango wa mashirika yasiyo ya Kiserikali (NGOs) katika kuchochea maendeleo katika Jamii, mkoa na Taifa kwa ujumla.
Ameyasema hayo wakati akisoma hotuba yake kwenye Mkutano wa Mashirika yasiyo ya Kiserikali Mkoa wa Ruvuma uliofanyika katika ukumbi wa Manispaa ya Songea.
"Ninatambua kazi kubwa mnayoifanya ya kushirikiana na Serikali katika kuwaletea maendeleo wananchi katika nyanja mbalimbali, niwapongeze na niwaombe muendelee kutupa ushirikiano katika utekelezaji wa shughuli mbalimbali zinazofanyika katika mkoa wetu," alisema Kanali Ahmed.
Kanali Ahmed ameyataka mashirika hayo kuhakikisha wanashirikiana vizuri na mamlaka za Serikali ikiwa ni pamoja na Wilaya, Halmashauri, pamoja na watendaji wa Kata na Tarafa, katika utekelezaji wa shughuli zao, lengo ni kuepusha changamoto zinazoweza kujitokeza, na kuhakikisha kuwa mipango yao inatambulika rasmi na taasisi husika za Serikali.
Naye Mwenyekiti wa Mashirika yasiyo ya Kiserikali Mkoa wa Ruvuma (NaCoNGO), Anthony Mbilinyi, amesema wajibu wa mashirika yasiyo ya Kiserikali ni kutoa huduma bora na stahiki katika jamii, kufuatilia sera na kuhamasisha mabadiliko ya kijamii na kuhakikisha shughuli zote zinazofanywa na mashirika hayo zinaendeshwa Kwa kuzingatia Sheria na maadili ya kitaifa na kimataifa.
Ametaja mafanikio ya mashirika hayo katika Mkoa wa Ruvuma kuwa ni kuwafikia wananchi wapatao 76,000 kupitia afua mbalimbali ambazo zimekuwa kichocheo cha maendeleo ya mkoa na kuboresha ustawi wa jamii ikiwa zaidi ya shilingi bilioni 2 zimetumika katika wilaya zote za mkoa kutekeleza miradi ya afya, kilimo, na maendeleo ya kijamii.
Kwa upande wake Msajili Msaidizi wa Mashirika yasiyo ya Kiserikali Mkoa wa Ruvuma, Xsaveria Mlimila, amesema katika Mkoa wa Ruvuma mashirika 192 yamesajiliwa kisheria na changamoto kubwa ni kukosekana kwa taarifa sahihi za mashirika hayo ambayo yamesajiliwa kisheria.
Amebainisha kuwa kwa mwaka wa fedha 2024/2025 mashirika hayo katika mkoa wa Ruvuma yamekuwa yakiendelea kutekelezeka miradi mbalimbali ya kijamii, kiuchumi na kiafya katika afua mbalimbali ikiwemo Elimu, lishe, kilimo, afya, mazingira pamoja na mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia ambapo walengwa 89,000 wamefikiwa.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: KERO PIGA 0800110174
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.