Taasisi isiyokuwa ya kiserikali ya St Teresa Orphans Foundation (STOF) imetumia zaidi ya shilingi milioni 7.9 kujenga kisima cha maji katika shule ya msingi Msamala iliyopo manispaa ya Songea mkoani Ruvuma.
Mkurugenzi wa STOF, Teresa Nyirenda, amesema wanafanya kidogo wanachokiweza kwa kuwa hawawezi kufanya zaidi ya Serikali lakini wanaunga mkono juhudi ambazo Serikali imekuwa ikizifanya.
Amebainisha kuwa kisima hicho kimegharimu shilingi milioni 7,985,000 ambapo fedha hizo zimewekezwa hapo ili kuwasaidia wanafunzi kupata maji salama ya kunywa na kutunza mazingira kwa kufanya usafi vyooni, madarasani na kumwagilia mimea.
Naye Mwalimu Mkuu wa shule ya msingi Msamala, Mwl. Kinyunyu, ameishukuru taasisi hiyo kwa msaada mkubwa wa kuwachimbia kisima, amesema sasa wataweza kuzuia magonjwa mbalimbali ya matumbo kwa kuwa vyoo vinakuwa safi muda wote, pia wanatumia maji hayo kunywa, kufanya usafi vyumba vya madarasa na ofisi kwa ufanisi.
Mwanafunzi wa shule hiyo, Christopher Mkumbo, amesema awali walikuwa wakipata changamoto hasa maji yakikata walikuwa wakishindwa kupikiwa chakula huku wakilazimika kubeba maji kutoka nyumbani, baada ya kuchimbiwa kisima sasa wataweza kutumia maji hayo katika shughuli mbalimbali shuleni hapo.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.