Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini Tanzania (TARURA) wilayani Mbinga, mkoani Ruvuma, umetenga zaidi ya shilingi milioni 468 kwa ajili ya kuendeleza mradi wa ujenzi wa Barabara ya Kihamili–Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga kwa kiwango cha lami.
Meneja wa TARURA Wilaya ya Mbinga, Oscar Mussa, amesema barabara hiyo yenye urefu wa kilomita 3.4 inajengwa kwa awamu, ambapo kwa mwaka wa fedha 2024/2025 imejengwa kwa kiwango cha lami urefu wa mita 750.
Mussa ameongeza kuwa mradi huo pia umetekeleza kazi ya kufungua barabara mpya yenye urefu wa kilomita 3.5 kuelekea makazi mapya ya viongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga.
Barabara hiyo inalenga kuondoa adha ya usafiri kwa wananchi wanaokwenda kupata matibabu, kurahisisha huduma za usafirishaji wa mazao, na kukuza uchumi wa wakazi wa Mbinga na taifa kwa ujumla. Pia, itawasaidia wanafunzi na wafanyakazi wa Chuo cha Ufundi Stadi (VETA) kufika na kurudi chuoni kwa urahisi.
Kwa mujibu wa Mussa, kazi zilizofanyika hadi sasa ni ujenzi wa barabara kwa tuta, huku mkandarasi akiendelea na ujenzi wa mitaro ya maji, uwekaji wa alama za barabarani na taa.
Mkazi wa kijiji cha Kigonsera, Benson Chiwinga, amepongeza serikali kwa kutekeleza miradi hiyo, akisema imewezesha vijana kupata ajira na ujuzi wa kujiajiri. Aidha, ameomba miradi zaidi iletwe katika Tarafa ya Kigonsera ili kuboresha maisha ya wananchi.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.