SERIKALI ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt.John Magufuli imetoa zaidi ya shilingi bilioni tatu kutekeleza mradi wa ujenzi wa jengo la ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo.
Akitoa taarifa ya mradi huo kwa Kamati ya Siasa ya CCM ya Mkoa wa Ruvuma,Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo Kassim Mpenda amesema mradi ulianza kutekelezwa mwaka 2017 na kwamba lengo la mradi ni kutatua changamoto ya uhaba wa ofisi unaowakabili watumishi wa Halmashauri hiyo na wananchi.
Hata hivyo amesema mradi unaendelea kujengwa kwa awamu tatu hadi sasa ambapo katika awamu ya kwanza mkataba ambao ulikuwa unatekelezwa na Mkandarasi Wakala wa Majengo Tanzania TBA,ulikuwa ni zaidi ya shilingi milioni 493,awamu ya pili ni mkataba wa zaidi ya bilioni mbili na awamu ya tatu ujenzi unafanyika kwa force akaunti kwa ajili ya umaliziaji wa asilimia 18 iliyobakia kukamilisha mradi.
“Mradi huu hadi sasa umepokea zaidi ya sh.bilioni tatu kutoka serikali kuu,kiasi cha zaidi ya sh. Bilioni 1.9 kimekwishatumika katika jengo hili,Mkandarasi TBA katika awamu zote mbili amelipwa zaidi ya bilioni 1.89’’,alisema Mpenda.
Hata hivyo amesema Mkandarasi TBA alisimamishwa kuendelea na kazi ya ujenzi na Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Christina Mndeme Juni 6 mwaka huu,baada ya Mkandarasi huyo kupata changamoto ya kufungiwa akaunti zake zote na kushinda kuendelea na kazi,hali iliyosababisha Halmashauri kutumia force akaunti kukamilisha mradi huo.
Amesema mradi wa jengo hilo hivi sasa upo katika hatua za umaliziaji ukiwa umefikia asilimia 82 kwa ujumla wake na kwamba mradi unatarajia kukamilika Agosti 30 mwaka huu.
Akizungumza mara ya kutembelea na kukagua mradi huo kwa niaba ya Kamati,Mwenyekiti wa Kamati ya Siasa ya CCM Mkoa wa Ruvuma Oddo Mwisho ameushauri uongozi wa Halmashauri hiyo kufanya kazi mchana na usiku ili kukamilisha kazi kwa sababu mradi huo umechelewa kukamilika na wananchi wanausubiri kwa hamu.
“Sisi Chama cha Mapinduzi tunataka wakati wa Kampeni Agosti mwaka huu tuwaambie wananchi wa Madaba kuwa tuliahidi,tumetekeleza kujenga jengo la Halmashauri,mkichelewa mtatuangusha’’,alisema Mwisho.
Hata mwisho kwa niaba ya wananchi wa Madaba amemshukuru Rais Magufuli kwa kutoa fedha ambazo zinatekeleza mradi huo mkubwa wa ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Madaba ambalo likikamilika litatatua changamoto kwa wananchi na watumishi.
Imeandikwa na Albano Midelo
Afisa Habari wa Mkoa wa Ruvuma
Julai 5,2020
Madaba
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.