PERAMIHO ILIVYOSHEHENI VIVUTIO VYA UTALII WA KIUTAMADUNI NA KIHISTORIA
Mji wa Peramiho uliopo Wilaya ya Songea Mkoa wa Ruvuma ni miongoni mwa miji ya zamani yenye historia ya kipekee katika ukanda ya kusini.
Mji wa huo unafahamika zaidi nje ya nchi pengine kuliko miji mingine iliyopo kusini mwa Tanzania kutokana na mji huo kuwa na historia ya namna yake kipekee ikiunganisha Tanzania na mataifa ya Ulaya.
Historia ya mji wa Peramiho uliopo kilometa 24 tu kutoka makao makuu ya mkoa wa Ruvuma Songea inaunganishwa na wabenediktini wa kanisa katoliki kutoka St.Otilia nchini Ujerumani, ambao waliamua kuweka makao makuu yao katika Abasia ya Peramiho.
Wabeneditine hao waliingia kwa mara ya kwanza katika mji huo mkongwe mwaka 1898 wakiongozwa na Kasian Spiss. Tangu wakati huo wabenediktine hao wamekuwa wakifanya mambo yanayoutangaza mji huo hali iliyosababisha kuutambua mji wa Peramiho kuwa ni mji unaokidhi vigezo kuwa mji wenye utalii wa kiutamaduni.
Mhifadhi Kiongozi wa Makumbusho ya Taifa Philipo Maligisu anasema wabenediktine wa Abasia ya Peramiho wametengeneza historia ya kipekee na kuvutia katika nchi ya Tanzania ambao wameacha historia katika mji wa Peramiho na taifa kwa ujumla hasa walipojikita katika suala zima la elimu na kuamua kuwekeza katika elimu kwa zaidi ya miaka 100 iliyopita.
Historia inaonesha kuwa walipoingia kwa mara ya kwanza wabenediktine hao kwa kutambua umuhimu wa elimu waliamua kuanzisha madarasa kwa kufundisha walimu na kufundisha wanafunzi hivyo kufundisha elimu zote mbili yaani elimu ya kiroho na elimu dunia
Kwa msingi huo eneo la Peramiho katika historia ya Tanzania ina historia ya kipekee kwa zaidi ya miaka 100 hivyo kuna ushahidi ambao unaonesha wabenediktine walidhamiria kufanya mambo ya msingi katika mji wa Peramiho na taifa kwa ujumla.
Utafiti uliofanywa katika mji wa Peramiho unaonesha kuwa wabenediktine hao walizindua rasmi mji huo Julai 31,1898 na tangu hapo waliendelea na shughuli zao wakiwa na mahusiano mazuri wakati huo na utawala wa machifu katika eneo hilo.
Hata hivyo mahusiano hayo mazuri baina ya wabenedikitine hao kutoka nchini Ujerumani na machifu ulikuja kuharibika wakati wa vita ya Majimaji ambayo vilianza mwaka 1905 na kumalizika mwaka 1907 na kusababisha padre Fransis Scuss wa Abasia hiyo kuuawa Septemba 9 1905.
Baada ya kumalizika vita hiyo, ilijitengeneza tena historia mpya ya kanisa la Abasia ya Peramiho hivyo kulichukulia eneo hilo kama eneo la kipekee kwa kuzingatia misingi ya sheria ya Tanzania namba 10 ya mwaka 1964 na maboresho yake namba 22 ya mwaka 1979 ambayo inayatambua maeneo yote ya kihistoria kulingana na umuhimu wake katika jamii.
Wananchi wa Ujerumani wanaijua Peramiho pengine kuliko hata sisi watanzania,ndiyo maana kizazi na kizazi wanasafiri kwa gharama kubwa hadi katika mji huo ili kufanya utalii wa kiutamaduni kwa kutembelea katika maeneo mbalimbali ya kihistoria ili kujifunza mambo mbalimbali.
Sera ya Taifa ya utamaduni ya mwaka 1997 ina tamka bayana kuwa eneo lolote la kihistoria linapokuwa limetimiza miaka 100 tayari moja kwa moja linaingia katika urithi wa utamaduni wa taifa.
Kutokana na hali hiyo ukiangalia mji huo wa Peramiho tayari umekidhi vigezo na maeneo yake yote ya kihistoria kuingia katika urithi wa utamaduni wa taifa kwa ajili ya kujifunza elimu na utalii.
Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia Idara ya Makumbusho ya taifa ipo katika mchakato wa kuliingiza eneo la Peramiho katika urithi wa utamaduni wa taifa na watu wengi watatembelea kwa lengo la kuhitaji kufanya utafiti,kujifunza na kujua nini kilichopo ndani.
Historia inaonesha kuwa wabenediktine walifikia katika mlima wa Peramiho miaka ya 1888 ambao waliamua kujenga kanisa la mwanzo nyuma ya hospitali ya Misheni ya Peramiho ambako hivi sasa kuna chuo cha uuguzi.
Kwa mujibu wa machapisho ya ujio wa wabenedikitine katika Abasia ya Peramiho,padre Kassian Spiss alifanya kazi Kurasini Dar es salaam mwaka 1893 na baadaye akahamishiwa Tosamaganga Iringa mwaka 1897 na hatimaye alitumwa kuanzisha misheni Songea Peramiho Julai 31,1898.
Baada ya muda padre Kassian alikwenda Songea kwa Mkuu wa Wilaya ili kufuatilia mashauri ambapo wakati anakwenda alipita njia ya mkato ili afike mlima Mbewike.Wakati anapita katika mlima Mbewike ndipo aligundua mahali pengine pazuri juu ya mlima Peramiho hatimaye akaamua kuanzisha misheni mahali hapo ndiyo Peramiho ya leo.
Kulingana na historia ya Peramiho Julai 31,1898 wamisionari walianza kujenga msingi wa kanisa dogo lenye urefu wa mita 13 na upana mita saba.
Ujenzi wa kanisa hilo ulianza mwaka 1902 hadi 1905, kanisa hilo lilijengwa katika mji wa Peramiho na nyumba nyingi za wamisionari ambapo Padre Kasian Spiss alikuwa ndiyo paroko wa kwanza wa Peramiho, Padre ambaye aliwekwa wakfu Novemba 16,1902 kuwa Askofu wa kwanza wa jimbo la Zanzibar kusini, makao makuu yake yalikuwa ni Peramiho na Kigonsera.
Kadri miaka ilivyozidi idadi ya wakristo iliendelea kuongezeka na kufanya kanisa hilo la mwanzo kuwa ndogo ndipo wabenedikitine hao waliamua kujenga kanisa kubwa jipya la sasa ambalo lina vivutio vingi adimu.
Kanisa la pili la Peramiho lina saa ya maajabu ambayo ilitengenezwa kwa vyuma zaidi ya miaka 78 iliyopita na wajerumani na kwamba tangu mwaka 1946 ilipotengenezwa hadi sasa saa hiyo haijawahi kusimama wala kupoteza majira jambo ambalo linawashangaza na kuwavutia wengi kutembelea kanisa hilo ili kuiona saa hiyo ya maajabu.
Kanisa kuu la Peramiho lilitumia matofali zaidi ya milioni tatu,ujenzi ulianza wakati Askofu Gallus Steiger na bruda Gisral Stumpf ambaye aliandaa mchoro wa kanisa hilo mwaka 1940 na mwaka 1941 msanii wa majengo Hans Burkard wa Uswis alisanifisha rasimu ya michoro hiyo na kumrejeshea Askofu Gallus mwaka 1943 na michoro kukamilishwa na bruda Gislar.
Kazi ya ujenzi wa kanisa hilo ilianza Julai 6,1943 na kumalizika Septemba 9,1943.Kenchi za mihimili ya kanisa kuu hilo zenye uzito wa tani tano chini ya usimamizi wa mabruda Nonosius Bleicher na Menas Leicht ilifanyika na kupandishwa kwa mashine maalum iliyotengenezwa na bruda Jucundus Weigele Agosti 1946.
Mnamo Novemba 24,1945 vigae vyote 120,000 vilikuwa tayari kwa ajili ya kuezekea kanisa hilo na mnamo mwaka 1948 kanisa kuu Peramiho lilibarikiwa na padre Heribert na padre Gerod Rupper akawa padre wa kwanza kuhubiri katika kanisa hilo jipya.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.