MBUNGE wa Jimbo la Mbinga mjini Jonas Mbunda,amekabidhi Sh.milioni 21,200,000 taslimu na vifaa vya ujenzi vyenye thamani ya Sh.milioni 31,944,000 vilivyonunuliwa kwa fedha za mfuko wa jimbo kwa mwaka wa fedha 2022/2023.
Fedha na vifaa hivyo zimetolewa ili kukarabati vyumba vya madarasa,zahanati,ofisi za serikali za vijiji,mitaa na kata zenye miradi inayoendelea kutekelezwa pamoja na ofisi za Chama cha Mapinduzi.
Akikabidhi fedha na vifaa kwa madiwani,watendaji wa kata na viongozi wa Chama cha Mapinduzi Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Mbinga Kelvin Mapunda kwa niaba ya Mbunge,amewataka viongozi hao kwenda kusimamia vizuri matumizi ya fedha hizo.
Mapunda,ametoa siku 21 kwa viongozi kuhakikisha fedha na vifaa hivyo vinafanya kazi iliyokusudiwa ili wananchi waone matokeo yake,badala ya kwenda kutumika kinyume na malengo yake.
Amempongeza Mbunge kwa kuwathamini na kuwajali wananchi wa jimbo hilo kutokana na utaratibu wake wa kufika kijiji hadi kijiji kwa ajili ya kusikiliza kero na changamoto zilizopo katika jamii na kuzitafutia majawabu.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Mji Mbinga Enock Ndunguru,ameipongeza ofisi ya Mbunge kwa matumizi sahihi ya fedha za mfuko wa Jimbo zinazoletwa na serikali ambazo zimesaidia sana kuchochea maendeleo ya wananchi na Jimbo hilo.
Ndunguru,amewataka wananchi kumpa ushirikiano Mbunge wao na kuunga mkono juhudi mbalimbali zinazofanywa na Serikali ya awamu ya sita iliyodhamiria kuboresha maisha ya wananchi wa jimbo la Mbinga mjini.
Kwa upande wake katibu wa Mbunge Simon Ponera,amemshukuru Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuongeza fedha za mfuko wa Jimbo la Mbinga mjini kutoka Sh.milioni 43 hadi milioni 58 na ongezeko hilo linatoa wigo mpana kwa ofisi ya Mbunge kutekeleza miradi mingi ya maendeleo.
Amesema,hatua ya Rais Samia Hassan kuendelea kutoa fedha za miradi mbalimbali katika jimbo hilo ikiwamo ujenzi wa vituo vya afya,vyumba vya madarasa,umeme,maji na miradi mingine ya maendeleo imesaidia sana kukuza kipato cha mwananchi mmoja mmoja,jimbo na wilaya ya Mbinga.
.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.