MKOA wa Ruvuma unatarajia kuzalisha zao la parachichi tani 37,500 ifikapo mwaka 2025.
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma kanali Laban Thomas amesema Mkoa umelenga kuongeza uzalishaji wa zao hilo kama yalivyo mazao mengine ya biashara kwa lengo la kuwawezesha wananchi kukuza uchumi kwa miezi ya Februari na Mei kila mwaka.
RC Thomas amelitaja lengo kuwa ni kuongeza uzalishaji wa parachichi kutoka hekta 2,446 zinazozalisha tani 1,769 hivi sasa na kufikia zaidi tani 37,000 mwaka 2025 na kwamba uzalishaji huo utafikiwa kwa kuweka mikakati itakayoongeza tija ya uzalishaji.
“Tija ya uzalishaji kwa eneo kwa sasa ipo chini ambapo uzalishaji kwa eneo la hekta moja ni tani 0.7228,miongoni mwa mikakati inayotekelezwa ili kuongeza uzalishaji wa zao la parachichi ni kuwezesha kuwaunganisha wakulima kupitia vikundi vya wakulima’’,alisema.
Mikakati mingine ameitaja kuwa ni kuwapatia wakulima mbegu za parachichi,kuwafundisha namna ya kuanzisha kitalu cha miche ya parachichi,kuwafundisha namna ya kubadi(grafiting),kuandaa shamba,kupanda na kuhudumia miche ya parachichi.
Kwa upande wake Afisa Kilimo ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Onesmo Ngao,amesema katika msimu wa mwaka 2021/2022 ,wakulima wamehamasishwa kulima zao la parachichi ambalo hivi sasa lina soko kubwa ndani ya nje ya nchi hasa katika nchi ya China ambayo ina mahitaji makubwa ya zao hilo.
Akizungumza mjini Songea hivi karibuni Balozi wa China nchini Tanzania Mheshimiwa Chen Mingjian alitoa rai kwa wakulima wa Mkoa wa Ruvuma kuongeza uzalishaji wa zao la soya na parachichi kwa kuwa soko la mazao hayo nchini China ni kubwa.
Uzalishaji wa zao la parachichi mkoani Ruvuma unafanyika katika wilaya za Songea,Mbinga na Nyasa.
Imeandikwa na Albano Midelo
Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Mkoa wa Ruvuma
Novemba 13,2022
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.