NYASA KUWA KANDA MAALUM YA KIUCHUMI KATIKA USHOROBA WA MTWARA
SERIKALI inatarajia kuanzisha Kanda Maalum ya kiuchumi {Special Economic Zone} katika eneo la Mbambabay ziwa Nyasa Wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma ili kuhakikisha bidhaa zote ambazo zinapatikana Kariakoo jijini Dar es salaam ziweze kupatikana Nyasa.
Hayo yamesema na Balozi wa Tanzania nchini Malawi Mheshimiwa Humphrey Polepole alipofanya ziara ya siku moja mkoani Ruvuma katika wilaya ya Nyasa kuangalia fursa za uwekezaji katika ushoroba wa Mtwara,unaonzia mkoani Mtwara hadi Mbambabay ziwa Nyasa.
Akizungumza baada ya kukagua bandari Kongwe ya Mbambabay na bandari mpya ya Ndumbi ambayo serikali imetoa zaidi ya shilingi bilioni 12 kujenga bandari hiyo,Balozi Polepole ametoa rai kwa wadau kuwa tayari kutumia fursa zote zinazopatikana katika ushoroba wa Mtwara.
“Ushoroba huu ni wa barabara inayotoka bandari ya Mtwara na inakuja kwa kilometa 822 mpaka bandari ya Mbambabay,ushoroba huu katika kusini mwa Afrika,ndiyo ushoroba bora zaidi na mfupi kuliko shoroba nyingine zote’’,alisema.
Amesema ushoroba wa Mtwara umesheheni madini ya aina mbalimbali yakiwemo makaa ya m awe,dhahabu,uranium na madini mengine ambayo ni fursa kwa wakazi wa eneo lote la ushoroba.
Polepole amesema wamedhamiria kuhakikisha ushoroba wa Mtwara unatangazwa na kuwa mbadala wa ushoraba wa Dar es salaam kwa sababu Dar es salaam hadi Lilongwe ni Kilometa 1600 wakati Ushoroba wa Mtwara ni kilometa 900.
Balozi huyo wa Tanzania nchini Malawi amesema kutokana na hali hiyo ametoa rai kwa Mamlaka ya Bandari Tanzania TBA kuboresha miundombinu ya bandari ziwa Nyasa ili serikali ivune pesa na kukusanya kodi kwenye ushoroba huu kutoka nchi za Malawi,Msumbiji,Zambia na Zimbabwe.
Amesema serikali ina mipango mikubwa ya kuwezesha usafirishaji wa shehena ya mizigo zaidi ya tani laki moja ambayo itawezesha milango ya kibiashara kufunguka katika bandari za Mtwara,Mbambabay,na ushoroba wote wa Mtwara.
Ametoa katika nchi ya Malawi tayari ubalozi umepokea maombi ya wafanyabiashara ambao wapo tayari kujiridhisha utayari wa ushoroba wa Mtwara ili waanze kupitisha shehena za mizigo kupitia ushoroba wa Mtwara.
”Sisi kama ubalozi wa Malawi,tumetoa ombi maalum kwa Mkoa wa Ruvuma hususan wilaya ya Nyasa,kuhakikisha tunaanzisha eneo maalum la kiuchumi ambalo linawezesha kupatikana bidhaa zote ambazo zinapatikana Kariakoo jijini Dar es salaam ziweze kupatikana Mbambabay’’,alisisitiza.
Amesema ili kuhakikisha suala hilo linafanikiwa kwa asilimia 100,meli ya abiria ya Mbeya II katika ziwa Nyasa hivi karibuni inatarajia kuanza safari za kuvuka ziwa kutoka Bandari ya Mbambabay Tanzania na Kwenda nchini Malawi katika bandari za Ntakabay,Chilumba na Chipoka ambako watafarishwa wafanyabiashara na mizigo kuja Mbambabay na kununua bidhaa mbalimbali zitakazokuwepo baada ya kuwa kituo cha kiuchumi.
Amesema bidhaa hizo zitakwenda nchini Malawi hadi Bandari ya Tete nchini Msumbiji kupitia ziwa Nyasa ambayo itakuwa ni fursa kubwa ya kibiashara wa Tanzania nan chi jirani.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas akizungumzia uwekezaji uliofanyika katika bandari ya Ndumbi,amesema serikali imewekeza mabilioni ya fedha kutekeleza mradi huo ambao umekamilika.
Amesema Mkoa umejiandaa kuanzisha maeneo maalum kwa ajili ya uwekezaji ambapo hivi sasa bidhaa zote ambazo zitahitajika katika nchi Jirani zitapatikana katika bandari ya Mbambabay ziwa Nyasa ili kupunguza umbali wa Kwenda Dar es salaam.
Ametoa rai kwa wafanyabiashara wa Tanzania kuchangamkia fursa hiyo na kwamba serikali ipo tayari kuwawezesha miundombinu yote inayohitajika ili bidhaa zote ziweze kupatikana katika wilaya ya Nyasa.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Mbinga ambaye pia ni Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Nyasa Mheshimiwa Aziza Mangasongo amesema kukamilika kwa mradi wa bandari ya Ndumbi kunafungua fursa mpya za uwekezaji mkoani Ruvuma.
Imeandikwa na Albano Midelo
Afisa Habari Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Ruvuma
Septemba 8,2022
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.