Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge amewaagiza viongozi na wadau wa vyama vya ushirika kusimamia mapato ya Halmashauri kupitia mazao yanayouzwa kwa mfumo wa stakabadhi ghalani kwa lengo la kuongeza maduhuli ya Serikali.
RC Ibuge ametoa maagizo hayo wakati wa kikao cha baraza la madiwani, cha kujadili Hesabu za Mkaguzi Mkuu wa Serikali kwa mwaka wa fedha 2019/2020, kilichofanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Songea mkoani Ruvuma.
Amesema kuwa, mapato ya Serikali yamekuwa yanapotea kwasababu ya usimamizi na ufuatiliaji mdogo, kwa baadhi viongozi kutosimamia ipasavyo mazao yanayopaswa kuuzwa kwa mfumo wa stakabadhi ghalani ,kitendo kinachosababisha Halmashauri kukusanya chini ya kiwango kilichokusudiwa
Amesisitiza kuwa Waheshimiwa madiwani na watendaji kusimamia kwa umakini mkubwa uuzaji na ununuzi wa mazao ya wakulima, ili waweze kuuza mazao hayo kwa bei yenye tija, ili wakulima waweze kunufaika na kilimo wanacholima badala ya kulanguliwa mazao yao na walanguzi na kusababisha kuvunjika moyo kwakukosa mwelekeo.
”Mazao yanauzwa kwa stakabadhi ghalani yatauzwa kwa mfumo huo kwakuwa ni mwongozo uliowekwa na serikali”,amsisitiza Balazi Ibuge.
Ameongeza kwa kusema kuwa usimamizi na ufuatilia soko la mnada wa stakabadhi ghalani, unasaidia serikali kukusanya mapato na wakulima kuuza mazao kwa bei yenye tija na faida kwao.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wakulima wa Halmashauri ya Wilaya ya Songea, Mkoani Ruvuma, wamesema wanakubaliana na mfumo huo wa stakabadhi ghalani unaowataka wakulima wa ufuta soya na mbaazi kuuza mazao hayo kwenye vyama vya msingi vya ushirika (AMCOS)
“Hatupingani na maamuzi ya serikali ila tunataka viwepo vituo vidogo vidogo vya kukusanyia mazao hayo na soko lifanyike mara mbili kwa wiki badala ya siku moja kwa wiki”, walisema wakulima hao.
Wamesema changamoto wanayokutana nayo katika mfumo huo ni kutembea umbali mrefu, gharama za kukodi vyombo vya usafiri kwa ajili ya kufikisha mizigo kwenye vyama vya msingi vya ushirika pamoja na kufanyika kwa mnada mara moja kwa wiki.
Kufuatia changamoto hiyo wameiomba serikali kuweka vituo vidogo vidogo vya kukusanyia mazao, karibu na maeneo kitendo ambacho kitawaondolea adha ya kutembea umbali mrefu, gharama za kukodi vyombo vya usafiri kwa lengo la kufikisha mazao, kwenye vyama vya ushirika sanjari na kuacha tabia ya kwenda kuuza mazao yao kwa walanguzi.
Mfumo wa stakabadhi ghalani ni mfumo ambao unawataka wakulima na wanunuzi kuuza mazao ya ufuta soya na mbaazi, kuuza mazao yao kwenye soko la mnada kwa bei ya makubaliano baina ya mnunuzi na mfanyabishara.
Imeandikwa na
Jacquelen Clavery
Afisa Habari Songea DC
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.