Katika tukio la kihistoria lililoshuhudiwa na maelfu ya wananchi, viongozi wa kitaifa, na wadau wa kimataifa, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, leo Julai 30, 2025, ameandika ukurasa mpya wa maendeleo kwa kuzindua Kiwanda cha Majaribio cha Kuchenjua Urani kilichopo katika eneo la Mkuju River, Wilaya ya Namtumbo, Mkoa wa Ruvuma.
Mradi huo wa kipekee, unaosimamiwa na kampuni ya Mantra Tanzania Limited kwa ushirikiano na kampuni ya kimataifa ya Rosatom kutoka Urusi, unatarajiwa kuwa miongoni mwa miradi mikubwa zaidi ya kimkakati si tu kwa Tanzania bali kwa Afrika Mashariki nzima.
Kiwanda hicho ni hatua ya mwanzo kuelekea uzalishaji mkubwa wa urani nchini – madini yenye mchango mkubwa katika sekta ya uzalishaji wa nishati ya nyuklia duniani.
“Leo tunashuhudia mwanzo wa enzi mpya ya kimaendeleo nchini – Tanzania sasa inaingia rasmi katika orodha ya mataifa yenye uwezo wa kuchakata na kutumia madini ya kimkakati kwa ustawi wa watu wake na maendeleo ya sayansi, teknolojia na diplomasia ya nishati,” alisema Dkt. Samia huku akishangiliwa na umati uliofurika katika eneo hilo la Mkuju River.
MWELEKEO WA MAGEUZI YA UCHUMI NA NISHATI
Kwa mujibu wa taarifa rasmi, mradi huu una thamani ya Shilingi Trilioni 3.06 na unatarajiwa kuanza uzalishaji rasmi mwaka 2026.
Mbali na kuchochea uchumi wa taifa, urani itatumika kama chanzo cha kuzalisha umeme wa nyuklia, hali itakayosaidia kupunguza utegemezi wa vyanzo vya kawaida vya nishati na kuiweka Tanzania kwenye ramani ya nchi zenye uwezo wa kuzalisha nishati endelevu kwa karne zijazo.
Waziri wa Madini, Mheshimiwa Anthony Mavunde, alibainisha kuwa mradi huu utafungua fursa nyingi kwa Watanzania, hususan vijana wa maeneo ya kusini mwa nchi kupitia ajira, uhamishaji wa teknolojia, na mafunzo ya kitaalamu ya usimamizi wa rasilimali za kimkakati.
“Uchimbaji wa urani si jambo la kawaida. Ni sekta ya juu yenye mahitaji makubwa ya utaalamu, ulinzi na ufuatiliaji wa kimataifa. Ndiyo maana tunahakikisha kwamba wazawa wanajengewa uwezo wa kisayansi na kiufundi kuendesha shughuli hizi kwa usalama na ufanisi,” aliongeza Waziri Mavunde.
URANI YA TANZANIA: AKIBA NA FURSA
Tanzania ni miongoni mwa nchi barani Afrika zenye akiba kubwa ya madini ya urani. Kwa mujibu wa Wizara ya Madini, urani imeshathibitishwa kuwapo katika maeneo mbalimbali ya nchi ikiwemo Bahi, Galapo, Minjingu, Mbulu, Simanjiro, Ziwa Natroni, Manyoni, Tunduru, Songea, Madaba, Nachingwea, na hususan Mkuju River wilayani Namtumbo.
Mara baada ya kuanza kwa uzalishaji katika mradi huu wa Mkuju River, Tanzania inatarajiwa kuwa nchi ya tatu barani Afrika kwa uzalishaji wa urani – nyuma ya Niger yenye akiba ya tani 200,000 na Namibia yenye tani 100,000. Niger, ambayo ndiyo kinara wa uzalishaji wa urani Afrika, ni miongoni mwa wazalishaji wakubwa wa dunia.
ATHARI CHANYA ZA MRADI KWA RUVUMA NA TANZANIA KWA UJUMLA
Kwa Mkoa wa Ruvuma, hii ni hatua kubwa ya kuibua fursa mpya za uwekezaji, uboreshaji wa miundombinu, biashara ndogondogo, pamoja na uimarishaji wa elimu ya sayansi na mazingira. Pia, mradi huu unatarajiwa kuwa kichocheo kikuu cha maendeleo ya kijamii na kiuchumi katika Wilaya ya Namtumbo na maeneo jirani.
Mbunge wa Jimbo la Namtumbo, Mhe. Vita Kawawa, hakuficha furaha yake akieleza kuwa ujio wa Rais Samia sio tu umetimiza ndoto ya muda mrefu ya wananchi wa Namtumbo bali umechochea matumaini mapya kwa vizazi vijavyo.
“Tunamshukuru Rais wetu kwa dhamira thabiti ya kulifikisha taifa kwenye uchumi wa viwanda kwa vitendo. Namtumbo sasa si historia tena – ni kitovu cha nishati ya Afrika Mashariki,” alisema kwa hisia kubwa.
Uzinduzi wa Kiwanda hiki ni alama ya mwanzo wa safari ya Tanzania kuelekea kuwa taifa linalotumia rasilimali zake kwa ufanisi, kwa maendeleo ya watu wake, bila kuathiri mazingira wala usalama
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: KERO PIGA 0800110174
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.