Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema mradi wa kiwanda cha majaribio cha kuchenjua madini aina ya urani katika wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma unaifanya Tanzania kuwa miongoni mwa nchi chache barani Afrika zinazochakata na kuongeza thamani rasilimali zake ndani ya nchi.
Akizungumza kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika kijiji cha Likuyu mara baada ya kuzindua mradi huo, Mhe. Dkt. Samia amebainisha kuwa Afrika inashikiliwa na asilimia 20 ya hifadhi ya madini aina ya urani na ni asilimia ndogo tu inayochakatwa ndani ya bara la Afrika.
"Tanzania itakuwa kwenye ramani ya duniani kama moja kati ya wachangiaji 10 wakubwa wa malighafi hii muhimu ya nishati safi, mradi huu wa majaribio ni sehemu ya utekelezaji wa dira yetu ya kuifanya Tanzania kuwa Taifa lenye viwanda na kufikia matarajio ya uchumi wa kati ngazi ya juu unaojitegemea,"alisema Mhe. Rais Dkt. Samia.
Ameeleza kuwa kiwanda hicho cha majaribio ni sehemu ya utekelezaji wa mikakati ya Serikali ya kuhakikisha madini hayo yanatumika kwa manufaa ya watanzania wote kwa kuzingatia usalama wa kiafya, kimazingira na kufuata viwango vya kimataifa.
Amesema tathimini iliyofanywa inaonyesha kuwa mradi huo itakuwa na uhai wa uzalishaji kwa zaidi ya miaka 20 na katika kipindi hicho Tanzania itapata faida mbalimbali ikiwemo uwekezaji wa fedha za kigeni unaokadiriwa kufikia dola za kimarekani bilioni 1.2 ( zaidi ya Trilioni 3 za kitanzania) na ajira kati ya 3,500 mpaka 4,000 huku ajira za kudumu zikiwa 750.
Mhe. Rais Dkt. Samia ameitaka kampuni inayotekeleza mradi huo ambayo ni Mantra Tanzania kuzingatia ushirikishwaji wa watanzania na wajibu wa kampuni kwa jamii ambapo amewataka kutoa ajira kwa watanzania hususan waliopo katika vijiji na eneo la karibu na mradi kwa ajira ambazo hazihitaji ujuzi mkubwa.
Kwa upande wake, Waziri wa Madini Mhe. Anthony Mavunde, amesema kuwa uzinduzi wa mradi huo ni hatua ya awali kuelekea ujenzi wa mtambo mkubwa wa uchenjuaji wa madini ya urani, akisisitiza kwamba katika nchi za Afrika Mashariki na Kati, hakuna mradi mwingine wa aina hiyo unaotarajiwa kujengwa wilayani Namtumbo.
Ameeleza kuwa mtambo huo utaiwezesha Tanzania kuwa miongoni mwa nchi tano pekee barani Afrika zinazomiliki mradi mkubwa wa uchenjuaji wa madini ya urani.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Kanali Ahmed Abbas Ahmed, amesema mradi huo unabeba matumaini makubwa ya mkoa na Taifa kwa ujumla, kwa kuwa unakadiriwa kuwa na mchango mkubwa katika kuongeza pato la Taifa, ajira kwa vijana na kuleta maendeleo ya kijamii na kiuchumi hasa katika sekta ya Elimu, Afya na Miundombinu.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: KERO PIGA 0800110174
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.