Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga, Joseph Kashushura, ametoa wito mzito kwa Watendaji wa Kata, Watendaji wa Vijiji na Wenyeviti wa Vijiji kushirikiana kwa karibu katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa lengo la kuongeza umiliki, kupunguza gharama na kuhakikisha miradi hiyo inatekelezwa kwa ubora unaotakiwa.
Rai hiyo imetolewa, wakati wa kikao kazi muhimu kilichowakutanisha Watendaji hao na Timu ya Menejimenti ya Halmashauri katika ukumbi wa Halmashauri hiyo, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya utekelezaji wa miradi iliyopokea fedha kutoka Serikali Kuu. "Hii miradi yetu, Serikali imeleta fedha kwa ajili ya utekelezaji. Naomba sana mkahamasishe wananchi kwenye maeneo yenu ili tushirikiane kwa pamoja," alisisitiza Kashushura.
Mkurugenzi huyo alifafanua kuwa, ili miradi ya maendeleo iwe endelevu, ni lazima wananchi wa maeneo husika washirikishwe kikamilifu tangu hatua za mwanzo. Alisema ushirikiano huo si tu huongeza umiliki wa miradi, bali pia huchochea ari ya wananchi kulinda na kuthamini rasilimali za umma. “Wananchi wakishiriki kwenye miradi, wanakuwa sehemu ya suluhisho, na mara nyingi huchangia nguvu kazi, vifaa na hata ulinzi wa miundombinu,” alisema.
Kwa upande wake, Claudius Miringa, Mwenyekiti wa Kijiji cha Mahilo Asili kutoka Kata ya Mbuji, alionesha kufurahishwa na hatua ya Halmashauri kuitisha kikao hicho muhimu. “Tangu nimechaguliwa sijawahi kushiriki kikao cha aina hii. Hii ni hatua kubwa ya uwajibikaji na ushirikiano. Naahidi kushirikiana kwa karibu na wananchi katika utekelezaji wa miradi,” alisema kwa msisitizo.
Naye Mtendaji wa Kata ya Lukarasi, Joseph Ndunguru, alisema kikao hicho ni chachu ya mabadiliko chanya katika utekelezaji wa miradi. Alisema kimewaongezea maarifa na kuelewa dhamira ya Serikali ya kuhakikisha wananchi wanahusishwa moja kwa moja katika miradi yote inayogusa maisha yao. “Kwa mtazamo wangu, huu ndio msingi wa maendeleo shirikishi tunayoyahitaji kwa sasa,” aliongeza.
Takwimu zinaonesha kuwa katika mwaka wa fedha 2025/2026, Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga imepokea zaidi ya shilingi bilioni 3.8 kutoka Serikali Kuu kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya elimu, afya, maji na miundombinu ya barabara katika kata zaidi ya 15. Fedha hizo zinalenga kuinua huduma za kijamii vijijini, na kushirikisha wananchi kutasaidia utekelezaji kwa wakati na kwa kiwango kinachotakiwa.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: KERO PIGA 0800110174
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.