WAZIRI wa nchi Ofisi ya Waziri Mkuu kazi,vijana,ajira na watu wenye ulemavu Prof. Joyce Ndalichako,ameziagiza Halmashauri zote hapa nchini kuhakikisha zinatenga fedha za kutosha kwa ajili ya kununua mahitaji ikiwemo mafuta kinga kwa watu wenye Ualbino.
Waziri Ndalichako ametoa agizo hilo katika Hotuba yake iliyosomwa na Mkuu wa wilaya ya Songea Kapenjama Ndile,wakati wa maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya uelewa kuhusu Ualbino ambayo kitaifa yamefanyika katika uwanja wa Majimaji mjini Songea.
Aidha Waziri Ndalichako alisema,kwa mwaka wa fedha 2022/2023 Serikali ilitenga Sh.milioni 50 kwa ajili ya mahitaji mbalimbali ikiwemo mafuta kwa watu wenye Ualbino.
Alisema,Serikali imewapa kipaumbele wenye ulemavu ikiwa ni pamoja na masuala ya elimu na uwezeshaji kichumi,afya,ajira,mafunzo ya ufundi stadi ili waweze kukabliana na changamoto katika maisha yao.
“Serikali ya awamu ya sita imeendelea na kutekeleza na kutoa huduma kwa watu wenye ulemavu nchini kwa kuzingatia sera,sheria,mikataba ya kikanda na Kimataifa na itaendelea kufanya hivyo wakati wote”alisema Ndalichako.
Alisema,serikali imeendelea kuboresha huduma za afya kwa kujenga vituo vya kutolea huduma za afya vyenye miudombinu rafiki kwa watu wote wenye ulemavu wa aina mbalimbali.
Mwenyekiti wa Tume ya haki za Binadamu na Utawala Bora Jaji Mstaafu Mathew Mwaimu,ameitaka Serikali kuongeza juhudi za kuwatambua watu wenye Ualbino na mahitaji yao kwa kutoa tiba na kinga ya saratani ya ngozi na kuweka mazingira mazuri kupitia mfumo wa utoaji wa huduma za afya nchini.
Ameishauri Serikali kupitia vyombo vya ulinzi na usalama, kufanya ukaguzi wa mara kwa mara katika maeneo mbalimbali ili kuzuia na kuchukua hatua juu ya vitendo vya unyanyasaji dhidi ya watu wenye ualbino.Amewaomba wananchi kushirikiana na serikali kukemea vitendo vya unyanyasaji na udhalilishaji na kutoa taarifa katika mamlaka husika juu ya vitendo hivyo dhidi ya watu wenye Ualbino katika maeneo yao.
Alisema,jitihada zaidi zinahitajika ili kuondoa kabisa changamoto za watu wenye Ualbino hususani ugonjwa wa saratani ya ngozi kwani kufanya hivyo kutawezesha ujumuishi wenye uimara wa kufurahi haki za binadamu.
Ameitaka jamii,kuunganisha nguvu kutokomeza saratani ya ngozi kwa watu wenye Ualbino ikiwemo kutoa elimu kwa kupinga vitendo vya udhalilishaji,unyannyasaji na mauaji ya watu wenye Ualbino.
Ametoa wito kwa watu kuachana na imani,mila,desturi na mitazamo potofu ambayo huwafanya watu wenye Ualbino kujiona hawakubaliki,hawawezi na hawana mchango wowote kwa jamii inayowazunguka na Taifa kwa ujumla katika shughuli zinazohusu maendeleo.
Katika hatua nyingine Jaji mstaafu Mwaimu,amewaasa watu wenye Ualbino kuzingatia miongozi ya afya juu ya kujikinga na saratani ya ngozi na kuchukua hatua za haraka kwa kwenda Hospitali pale wanapohisi wana vidonda kwenye miili yao.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Shirikisho la vyama vya wenye ulemavu nchini Ernest Kimaya alisema,kama shirikisho la watu wenye ulemavu wameanza kukaa pamoja ili kutatua changamoto zinazowakabili katika maisha yao ya kila siku.
Kimaila,ameishukuru serikali ambayo kuanzia mwaka 2012 imetoa ajira zaidi 214 kwa watu wenye ulemavu,hata hivyo ameiomba kuendelea kutoa kipaumbele kwa jamii ya watu wenye ulemavu.
Naye Mkurugenzi wa Kinga kutoka Taasisi ya Saratani ya Ocean Road Crispin Kahesa alisema, kati ya saratani zinazoongoza kwa watu wenye Ualbino ni saratani ya ngozi.
Alisema,kwa muda wa siku tatu wamefanikiwa kufanya uchunguzi kwa watu 370 ambapo kati ya hao watu 4 wameonekana na viashiria vya saratani na kutakiwa kwenda Hospitali ya Ocean Road kwa uchunguzi zaidi.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.