Na Albano Midelo,Songea
IDADI ya abiria wanaosafiri kwa Ndege za ATCL kwa kutumia kiwanja cha che Ndege cha Songea mkoani Ruvuma inaongezeka kwa kasi na kufikia abiria 18,580 katika kipindi cha mwaka 2023 hadi 2024.
Meneja wa Kiwanja cha Ndege Songea Dastan Komba,akitoa taarifa kwa Naibu Waziri wa Uchukuzi Mheshimiwa David Kihenzile amesema idadi hiyo ya abiria imetokana na miruko ya ndege 468 ilifanyika katika kiwanja hicho katika kipindi cha mwaka 2023 hadi 2024.
Amesema kiwanja cha ndege cha Songea kinahudumia ndege za ATCL zinazofanya safari mara tatu kwa wiki zenye uwezo wa kubeba abiria 70 na kwamba kiwanja hicho pia kinahudumia ndege za dharura.
Kulingana na Meneja huyo takwimu za idadi ya abiria katika kiwanja hicho zinaonesha kuwa kuanzia mwaka 2019 hadi 2021 idadi ya abiria walikuwa ni kati ya 2,020 hadi 3,971 na kwamba kuanzia mwaka 2021 hadi 2022 idadi ya abiria ilifikia 13,048 na mwaka 2023 idadi ya abiria ilifikia 18,580.
“Hadi kufikia Januari mwaka huu tumehudumia abiria 11,925, tunarajia hadi kufikia Juni mwaka huu kufikisha abiria 20,000 hili ni ongezeko kubwa sana la abiria lililotokana na kuanza kwa safari za ATCL hapa Songea kufuatia ukamilishaji wa miundombinu ya kiwanja’’,alisema Komba.
Hata hivyo amesema idadi ya abiria hivi sasa ni kubwa ukilinganisha na miruko ya ndege hivyo ATCL inatakiwa kuangalia uwezekano wa kuongeza miruko ya ndege ili kukidhi mahitaji ya abiria ambao wanaongezeka kwa kasi.
Akizungumzia uboreshaji uliofanywa na serikali katika uwanja huo,Meneja wa Kiwanja hicho amesema serikali imetoa zaidi ya shilingi bilioni 37 kupanua na kukarabati uwanja huo ambao utekelezaji wake umefikia asilimia 100
Amezitaja kazi zilizofanyika kwenye uboreshaji huo ni ukarabati na upanuzi wa barabara ya kutua na kurukia ndege kutoka meta 1625 hadi meta 1860 na upana wa meta 30,ujenzi wa eneo la usalama,ujenzi wa jengo la kuongozea ndege na ujenzi wa kituo cha nishati.
Kazi nyingine amezitaja kuwa ni usimikaji wa taa za kuongozea ndege,kufungwa taa za kuruhusu ndege kutu ana kuruka usiku na ujenzi wa uzio wa usalama.
Akizungumza baada ya kukagua na kupata taarifa za mradi huo,Naibu Waziri wa Nishati Mheshimiwa David Kihenzile ameupongeza uongozi wa kiwanja hicho kwa kupata hati ya kiwanja na kukamilisha ujenzi wa uzio kwa ajili ya usalama ambapo amewaagiza mameneja wengine wa viwanja vya ndege nchini kuiga mfano kutoka kiwanja cha Songea.
Hata hivyo Naibu Waziri huyo, kutokana na kusuasua kwa ujenzi wa jengo la abiria katika kiwanja cha Ndege cha Songea,ameiagiza Mamlaka ya Viwanja vye Ndege kuvunja mara moja mkataba na Mkandarasi aliyekuwa anajenga jengo na kumpa Mkandarasi mwingine.
“Serikali haiwezi kuendelea kuwavumilia watu ambao wanapewa kazi halafu hawakamilishi kwa wakati,atafutwe Mkandarasi mwingine arekebishe jengo la abiria lenye uwezo wa kuchukua abiria 150 kwa wakati mmoja ili lianze kutumika’’,alisisitiza.
Hata hivyo Kihenzile ameiagiza Mamlaka ya Viwanja vya Ndege kuweka malengo ya muda ya mrefu ya kuanza mchakato wa kujenga jengo kubwa la kisasa la abiria lemye hadhi na linaloendena na Mkoa wa Ruvuma.
Akizungumzia changamoto ya kuongezeka kwa abiria katika kiwanja cha Ndege cha Songea,Kihenzile amesema baada ya maboresho ya kiwanja hicho idadi ya abiria inaongezeka kwa kasi hivyo ameiagiza ATCL kuangalia uwezekano wa kuongeza miruko ya ndege itakayokidhi idadi ya abiria ambapo amesema ikiwezekana ndege zitue wiki nzima.
Kiwanja wa ndege wa Songea ni miongoni mwa viwanja 58 vya ndege vinavyosimamiwa na ATCL ambacho kilianza kujengwa kati ya mwaka 1974 na kukamilika mwaka 1980.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.