Wananchi wa Wilaya ya Mbinga wametakiwa kuzingatia ulaji unaofaa na unaojumuisha makundi matano muhimu ya vyakula na matumizi ya mbolea za asili ikiwa ni jitihada za kutokomeza tatizo la udumavu na utapiamlo mkali Wilayani humo.
Hayo yamebainishwa leo Machi 31 wakati wa kikao cha Tathmini ya Utekelezaji wa Mkataba wa Lishe kilicholenga kujadili hali ya lishe ndani ya Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga kwa kipindi cha kuanzia Oktoba hadi Machi 2020/2021 kilichofanyika katika Ukumbi wa Shule ya Sekondari Kiamili na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali ngazi ya Wilaya, Kata, mashirika yasiyo ya kiresikali, viongozi wa dini na wadau wengine wa lishe.
Katika kikao hicho cha Tathmini ya Utekelezaji wa Mkataba wa Lishe kilichoongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Mbinga, Mhe. Cosmas Nshenye imeelezwa kuwa takribani 2% ya watoto waliopo Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga wana udumavu na utapiamlo mkali huku 98% ya watoto wakiwa na hali nzuri ya lishe, ushauri ukitolewa juu ya ulaji wa vyakula unaozingatia makundi matano ambayo ni wanga, protini, mbogamboga, mafuta na sukari hasa ya asili, na matunda mchanganyiko sambamba na udhibiti wa matumizi ya mbolea za viwandani ikiwa ni hatua muhimu na madhubuti katika mapambano dhidi ya udumavu na utapiamlo mkali Wilayani humo.
Akizungumza wakati wa Tathmini hiyo Mhe. Nshenye ametoa wito kwa viongozi wote wa ngazi ya Wilaya, Kata na Vijiji, wadau mbalimbali na wananchi kushirikiana kwa pamoja ili kuwa na jamii yenye uwezo wa kutoa maamuzi juu ya suala la lishe na kwamba kwa sasa ni vema jamii ikaelimishwa juu ya matumizi ya mbolea za asili (mboji na samadi) na kushirikishwa kwa ukaribu zaidi kwa maafisa ugani na idara ya kilimo katika jitihada za kupunguza matumizi ya mbolea za viwandani, lakini pia kuongeza matumizi ya chokaa kama ilivyopendekezwa na tafiti mbalimbali za hali ya udongo zilizofanyika Wilayani Mbinga.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga, Bw. Juma Mnwele amesema ataendelea kusimamia uwajibikaji wa kila mmoja na kwamba hatosita kuwachukulia hatua ikiwa ni pamoja na kuwabadilisha vituo vya kazi wale wote watakaoonekana kusuasua katika mapambano dhidi ya utapiamlo na udumavu na kuboresha hali ya lishe kwenye maeneo yao suala ambalo pia linatekelezwa kitaifa kote nchini.
Kwa upande wao wajumbe waliohudhuria kikao hicho wamesema wao kama wadau muhimu tathmini hiyo imewapata fursa ya kujipima na kuona walipotoka, walipo na wapi wanaelekea katika mkakati wa kutokomeza hali ya udumavu na utapiamlo nchini na kuahidi kushirikiana kwa pamoja kufanyia kazi mapungufu na changamoto zote zilizobainishwa wakati wa kikao hicho.
Kikao cha Tathmini ya Utekelezaji wa Mkataba wa Lishe kimefanyika hufanyika kila robo kufuatia kusainiwa kwa mkataba huo kuanzia ngazi ya Taifa, Mkoa, Wilaya, Halmashauri, Kata na Vijiji lengo likiwa kufanya suala la lishe kuwa mtambuka sio la Idara na Wizara ya Afya pekee na kwamba ushiriano wa pamoja unahitajika ili kutoa huduma za lishe kwa jamii.
Imeandikwa na Salum Saidi
Afisa Habari Halmashauri ya Mbinga
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.