Benki ya NMB imetoa jumla ya madawati 191 yenye thamani ya shilingi milioni 15 katika shule mbili za sekondari wilaya ya Mbinga na shule moja ya msingi wilaya ya Songea mkoani Ruvuma.
Meneja wa NMB Kanda ya Kusini Janeth Shango amezitaja shule za sekondari zilizopata msaada huo kuwa ni Mbambi na Makita ambazo zimepata jumla ya madawati 134 yenye thamani ya shilingi milioni kumi ambapo kila shule imepata madawati 67.
Shango amesema NMB pia imetoa madawati 57 kwa shule ya msingi Mfaranyaki yenye thamani ya shilingi milioni tano.
“Kwa zaidi ya miaka saba mfululizo NMB tumechangia asilimia moja ya faida yetu kama sehemu ya uwajibikaji kwa jamii inayotuzunguka,kwa mwaka 2020,NMB imetenga zaidi ya shilingi bilioni moja kwa ajili ya kuchangia maendeleo ya jamii’’,alisisitia Shango.
Hata hivyo amesema NMB imejikita zaidi kwenye miradi ya elimu kuchangia madawati na vifaa vya kuezekea na katika sekta ya afya kuchangia vitanda na magodoro yake.
Akizungumza baada ya kupokea msaada wa madawati 134,Mkuu wa Wilaya ya Mbinga Cosmas Nsenye ameipongeza NMB kwa msaada huo ambao amesema umesaidia kupunguza changamoto ya madawati katika shule za sekondari Makita na Mbambi.
Amesema msaada huo utaongeza ufaulu kwa sababu wanafunzi watasomea katika mazingira rafiki ambapo amesisitiza kuwa NMB ni wadau wakubwa wa maendeleo nchini.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Songea Pololet Mgema akizungumza baada ya kupokea msaada wa madawati 57 katika shule ya msingi Mfaranyaki amesema Benki ya NMB imekuwa msaada mkubwa katika shule za msingi,sekondari na vituo vya kutolea huduma za afya.
Mgema amesema kila mwaka NMB imekuwa inatoa misaada wilayani Songea ambapo ametolea mfano mwaka jana,NMB ilitoa msaada vitanda,magodoro na mshuka vyenye thamani ya milioni kumi katika kituo cha Afya Madaba.
Amesema NMB pia ilitoa viti na meza katika sekondari ya Wino Halmashauri ya Madaba vyenye thamani ya milioni kumi na kwamba NMB pia ilitoa mabati zaidi ya 170 kwa ajili ya shule ya msingi Ndelenyuma katika shule hiyo.
Majidu Ngonyani ni Mwalimu Mkuu shule ya msingi Mfaranyaki ambapo amesema msaada wa madawati 57 uliotolewa na NMB utawafanya wanafunzi wote 650 kukaa kwenye madawati na kujifunza kwa furaha.
“Msaada huu utapunguza utoro na kuongeza ufaulu katika shule yetu,jukumu letu sasa ni kuhakikisha madawati haya yanatunzwa vizuri’’,alisema Ngonyani.
Restuta Ngonyani ni mwanafunzi wa sekondari ya Mbambi ameipongeza NMB kwa msaada huo wa viti na meza ambapo ametoa rai kwa wadau wengine wa maendeleo kuiga mfano wa Benki ya NMB.
Imeandikwa na Albano Midelo
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.