ASILIMIA 75 ya hali ya barabara katika Halmashauri ya Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma zina hali nzuri.
Kaimu Meneja wa TARURA katika Manispaa ya Songea Mhandisi Henry Mtawa amesema barabara za Manispaa ya Songea zina jumla ya kilometa 390.88 ambazo ni sawa na asilimia 17.1 ambazo zina hali ya kuridhisha na kwamba kilometa 40.62 ambazo ni sawa na asilimia 7.8 zina hali mbaya.
Mhandisi Mtawa akitoa taarifa ya TARURA kwenye Baraza la madiwani la Manispaa ya Songea, amesema katika mwaka wa fedha wa 2019/2020 Halmashauri ya Manispaa hiyo imetengewa zaidi ya bilioni 1.398 ili kufanyia matengenezo mtandao wake wa barabara.
“Matengenezo ya kawaida,zimetengwa zaidi ya shilingi milioni 342 ambazo zitatengeneza barabara za jumla ya kilometa kilometa 152.46’’,alisema.
Kulingana na Mhandisi huyo,fedha ambazo zimetengwa kwa ajili ya matengenezo ya barabara korofi zenye urefu wa kilometa 28.13 ni zaidi ya milioni 181 na kwamba matengenezo ya muda maalum zimetengwa zaidi ya milioni 670.
Amezitaja fedha ambazo zimetengwa kwa ajili ya madaraja ni milioni 95 ambazo zitatumika kujenga madaraja madogo mawili na kufanyia matengenezo daraja moja na kwamba Manipaa ya Songea katika kipindi cha mwaka 2019/2020 imetenga shilingi milioni 324 za fedha za maendeleo kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya Tunduru-Seedfarm yenye urefu wa kilometa 0.75 kwa kiwango cha lami nyepesi.
Hata hivyo amezitaja changamoto za barabara za vijijni na mijini katika Manispaa ya Songea kuwa ni ufinyu wa bajeti ya matengenezo ya barabara ambapo ili kukabiliana na changamoto hiyo inatakiwa kuongeza bajeti ya matengenezo ili kuendana na uhalisia wa mahitaji ya matengenezo.
Wakizungumza baada ya kupokea taarifa baadhi ya madiwani wametoa rai kwa TARURA kushughulikia haraka kero ya barabara katika Manispaa hiyo ambazo zimeharibika kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha hali ambayo imekuwa kero kubwa kwa wananchi.
Imeandikwa na Albano Midelo
Afisa Habari Mkoa wa Ruvuma
Februari 21,2020.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.