SERIKALI ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt John Magufuli imetoa zaidi ya shilingi biilioni tatu kwa Halmashauri ya Mji wa Mbinga mkoani Ruvuma kwa ajili ya ujenzi wa majengo tisa.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Mbinga Grace Quentin ametoa taarifa ya miradi hiyo kwa Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Christina Mndeme alipokagua miradi hiyo ikiwemo nyumba ya Mkurugenzi iliyogharimu sh.milioni 300,nyumba saba za wakuu wa Idara zimegharimu sh.milioni 350 na jengo la Halmashauri limegharimu sh.bilioni 2.9 ambalo limekamilika na kuanza kutumika.
Akizungumzia mradi wa nyumba za watumishi na nyumba ya Mkurugenzi ambayo itakuwa na ghorofa moja,Quentin amesema mradi kwa ujumla wake umefikia asilimia 70 na kwamba mradi ulianza kutekelezwa Aprili na unatarajia kukamilika Juni 2020.
“Mradi huu wa nyumba za watumishi utasaidia sana wakuu wa Idara,badala ya Halmashauri kuwalipa pango la nyumba,tutakuwa tumewasaidia nyumba hizi,mradi unafanyika kwa force account na Msimamizi Mkuu wa mradi ni TARURA’’,anasema Quentin.
Akizungumza baada ya kukagua miradi hiyo,Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Christina Mndeme kwa niaba ya wananchi wa Mbinga,amemshukuru Rais Dkt John Magufuli kwa kuruhusu kiasi hicho cha mabilioni ya fedha yaliyowezesha kujengwa jengo bora la Halmashauri ya Mji wa Mbinga.
“Tuna kila sababu ya kumshukuru Rais wetu kwa zawadi hii kubwa,kwa niaba ya serikali nawapongeza wana Mbinga Mji kwa kupata jengo hili zuri na rafiki la kutolea huduma’’,alisisitiza.
Amesema kiasi hicho cha fedha kimejenga majengo tisa,moja la Halmashauri likiwa limekamilika na majengo mengine nane yakifikia asilimia 70 ya ujenzi ambapo amesisitiza kuwa kazi ni nzuri ambapo ameahidi kuzipeleka Halmashauri nyingine kwenda kujifunza katika Halmashauri hiyo.
Hata hivyo amesema katika Mkoa wa Ruvuma anasimamia ujenzi wa majengo matatu ya Halmashauri yakiwemo Halmashauri ya Nyasa,Madaba na jengo la Mbinga Mji ambalo licha ya ujenzi wake kuanza nyuma limekamilika kabla ya waliotangulia kuanza ujenzi.
Amesisitiza kuwa Halmashauri ya Mji wa Mbinga wamekuwa mfano katika Mkoa kwa kukamilisha kazi na kuzishinda Halmashauri nyingine zilizopata fedha mapema na kuanza kazi mapema ambapo hadi sasa ujenzi wao haujakamilika hadi ameamua kuwapelekwa TAKUKURU kuchunguza.
Amemwagiza Mkurugenzi kuhakikisha kuwa jengo nzuri liwahudumia wananchi vizuri na kutoa maamuzi mema kwa manufaa ya wananchi wa Mji wa Mbinga na Tanzania.
IMEANDIKWA NA ALBANO MIDELO
AFISA HABARI WA MKOA WA RUVUMA
MEI 27,2020
MBINGA
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.