CHAMA cha Ushirika cha msingi kimuli,kilichopo kijiji cha Utiri, kata ya Utiri Wilayani Mbinga mkoani Ruvuma, kimetoa sh. milioni 100, kwa kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo katika kata ya Kitanda, Utiri na Kihangi mahuka.
Hayo yamesemwa na Meneja wa Chama hicho Ernest Komba, wakati akisoma Taarifa ya utendaji kazi wa Chama hicho, Katika Ziara ya kukagua Shughuli za Chama hicho cha Msingi iliyofanywa na Viongozi wa Chama kikuu cha Ushirika Mbinga (MBIFACU) na viongozi wa ushirika ngazi ya Mkoa wa Ruvuma.
Komba amesema kuwa fedha hizo zilizotolewa na Chama cha kimuli, zilitokana na mapato ya premium na ziada, za Ndani na kusaidia ukarabati wa majengo ya Taasisi za elimu na Afya, zilizomo katika maeneo yanayohudumiwa na Chama cha kimuli.
Ameitaja miradi iliyopewa fedha na chama hicho kuwa ni Zahanati ya Lipumba sh. milioni 14 ,Zahanati ya Kitanda milioni 9.5, Zahanati ya Utiri milioni saba na Sekondari ya Ndela milioni 15.
Miradi mingine ni Sekondari ya Kihangi Mahuka milioni 13, Sekondari ya Luli milioni 2.5, Sekondari ya Ngwilizi milioni 1 ,na Shule za Msingi 10 zilizoko katika Kata ya Utiri na Kitanda, ambazo zimepewa milioni 26.
Amesema awali wananchi walikuwa wakichangia fedha za mifukoni, au kusubiri miradi itekelezwe na Serikali. Lakini kwa sasa Chama kimeona ni vema kufanya maendeleo hayo ili kurudisha fadhila kwa wananchi ambao huuza mazao katika chama cha msingi ambapo hivi sasa wananchi wanaona faida ya uwepo wa chama cha Ushirika cha Msingi Kimuli.
“Chama kimetoa faida yake kwa kuchangia utekelezaji wa miradi mbalimbali, ya Afya na elimu kwa kuchangia ukarabati na ujenzi wa madarasa kutokana na uhitaji wa taasisi husika, ili kuamsha ari kwa jamii na watambue umuhimu wa chama chao cha Ushirika, kwa kuwa kama sio chama kutoa kiasi hicho basi wangelazimika kuchangia au kusubiri Serikali itoe fedha za kutekeleza miradi hiyo ya Maendeleo”, Alisema Komba.
Komba ametoa rai kwa Wananchi wa kata zilizo katika mradi, huo wajiunge na Chama cha ushirika na Msingi Kimuli kwa Maendeleo ya kaya na Jamii kwa ujumla.
Licha ya kuchangia miradi ya maendeleo,Meneja huyo amezitaja, huduma zingine zinazotolewa kuwa ni mradi wa Mashine ya kusaga nafaka ambao hutoa huduma kwa wanachama, lengo likiwa ni kupata uzoefu na kupata uzoefu wa kuanzisha kiwanda cha kuchakata unga wa mahindi ambapo hivi sasa chama kina mashine tatu katika Vijiji vya Utiri Mtama na Kitanda.
Kulingana na Meneja huyo Chama cha Ushirika cha Kimuli kimeanzisha Mradi wa Mashamba ya miti ambapo mpaka sasa tayari wameshapanda ekari 30 za miti katika kijiji cha Kitanda, mahande na Mtama lengo likiwa ni kuwa ni kitega uchumi kitakachoongeza mapato katika chama hicho hapo baadaye.
Ili kuhakikisha wakulima wa kahawa wanaongeza uzalishaji wa zao la kahawa Komba amesema Chama kimekuza miche bora ya kahawa(Compact) ili kukuza hali ya uzalishaji wa zao hilo ambapo Katika Msimu huu Chama kimepanda miche ya kahawa 120,000.
Amesema miche hiyo imeoteshwa kitaluni na kuwauzia wakulima kwa bei rahisi ili wakulima waweze kuzalisha Kahawa bora.Pia chama kina mradi wa usafirishaji mizigo kwa kutumia magari ya Chama kwa lengo la kusafirisha mbolea,kahawa na vifaa vya ujenzi, ili kuongeza pato la Chama.
Kwa mujibu wa Komba,Chama hicho cha ushirika pia hukusanya Mazao ya wanachama na ya wakulima wengine kuyachakata na kuyatafutia soko la ndani na nje ya nchi ili kjuimarisha ushirika.
Kaimu Meneja wa Chama Kikuu cha Ushirika Wilaya za Mbinga na Nyasa(MBIFACU) Henerck Ndimbo amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania John Magufuli kwa kuviongezea nguvu vyama vya Ushirika na Msingi kwa kuwa kwa sasa wakulima wengi mara baada ya kupata Elimu ya Ushirika wanauza mazao yao kupitia vyama vya ushirika na kupata manufaa mengi ikiwemo kusomesha watoto kununua pembejeo na kukuza pato la familia.
Kwa upande wake Mrajisi Msaidizi wa Vyama vya Ushirika Mkoa wa Ruvuma Bumi Masuba amekipongeza MBIFACU kwa kusimamia vema Vyama vya Msingi hali ambayo imewezesha kuimarisha ushirika kuanzia vyama vya msingi ambapo ametoa rai kwa wananchi kuvitumia Vyama vya Ushirika vya Msingi vilivyoko katika Maeneo yao.
Mkoa wa Ruvuma wenye wilaya tano na Halmashauri nane una jumla ya vyama vya ushirika 296 kati ya hivyo Halmashauri ya Wilaya ya Songea kuna vyama 31,Hamashauri ya Mbinga 81,Namtumbo 59,Nyasa 15,Manispaa ya Songea 24,Tunduru 48,Halmashauri ya Madaba 8 na Halmashauri ya Mji Mbinga 27.
Imeandikwa na Albano Midelo
Afisa Habari Mkoa wa Ruvuma
Julai 12,2020
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.