KUTOKANA na virusi vya corona vinavyoendelea kuisumbua dunia, Wizara ya Utalii na Maliasili imesema mapato katika sekta hiyo yameshuka kutoka Sh trilioni 2.6 zilizotarajiwa kukusanywa hadi kufikia Sh milioni 598.
Pia taasisi zilizokadiriwa kukusanya zaidi ya Sh bilioni 132.1 zinatarajia kukusanya Sh bilioni 33.5 ikiwa ni anguko la asilimia 75.
Vilevile, Serikali imesema kama hali haitatulia hadi Oktoba, ajira za moja kwa moja katika sekta ya utalii zitashuka kutoka 623,000 hadi kufikia 146,000 na watalii watashuka kutoka 1,867,000 waliotarajiwa hadi 437,000.
Kauli hiyo ilitolewa bungeni jana na Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla wakati akiwasilisha bungeni makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2020/21.
Dk. Kigwangalla alisema sekta ya utalii imeathirika kwa kiwango kikubwa kutokana na corona.
“Moja ya sekta muhimu zilizoathiriwa ni utalii. Sekta hiI kabla ya madhara hayo ilikuwa inachangia asilimia 25 katika mapato yote ya kigeni inayopata nchi yetu.
“Sekta hii imeathiriwa zaidi kutokana na ukweli kwamba inategemea zaidi mapato ya watalii wanaotoka nje ya nchi, ambao kwa sasa kutokana na ugonjwa huu, wameshindwa kusafiri na wengi wao wamesitisha safari za kuja nchini kutalii,” alisema Dk. Kigwangalla.
Alisema wizara ilifanya tathmini ya awali (rapid assessment) iliyojikita katika kipindi cha tangu ugonjwa huo uanze hadi Aprili 6, mwaka huu.
Dk. Kigwangalla alisema tathmini hiyo ilibaini kuwa madhara makubwa ya corona katika sekta ya utalii yalianza kuonekana mwanzoni mwa Machi, tofauti na Februari na Januari, mwaka huu ambapo hali ilikuwa shwari. Alisema tathmini ilibaini mashirika 13 ya ndege yalisitisha safari za kuja nchini tangu Machi 25, mwaka huu hivyo kuondoa uwezekano wa kuendelea kupata watalii kutoka nje ya nchi.
Dk. Kigwangalla alisema mashirika yaliyositisha safari zake ni pamoja ni Emirates, Swiss, Oman Air, Turkish, Egyptian Air, South African Airways, Rwandair, Qatar, Kenya Airways, Uganda Airlines, Fly Dubai na KLM.
“Vilevile, kampuni yetu ya ndege ya Air Tanzania imesitisha safari za nje ya nchi.
“Madhara haya yanaonekana kuwa makubwa zaidi ambapo tayari kuna dalili za kushuka kwa mapato yaliyotarajiwa kukusanywa na taasisi kubwa zilizo chini ya wizara ambazo ni Tanapa (Mamlaka ya Hifadhi za Taifa), NCAA (Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro), TFS (Wakala wa Huduma za Misitu) na Tawa (Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania).
“Kwa mfano, katika mwaka 2020/2021 Tanapa ililenga kukusanya Sh bilioni 363.9, lakini kutokana na hali inavyoendelea, makisio sasa yanakadiriwa kuwa Sh bilioni 64 au chini ya hapo,” alisema Dk. Kigwangalla.
Alisema NCAA ilikadiria kukusanya Sh bilioni 162.7, kwa sasa itakusanya Sh bilioni 58, TFS ilikadiria Sh bilioni 153.6, sasa ni Sh bilioni 121 na Tawa ilikadiria Sh bilioni 58.1 sasa ni Sh bilioni 22.
“Upungufu huo wa mapato ni mkubwa kwa sekta, na unaweza kusababisha baadhi ya taasisi za uhifadhi zilizo chini ya wizara kushindwa kujiendesha ikiwa ni pamoja na kulipa mishahara.
“Katika kukabiliana na hali hiyo, wizara imeendelea kuwashirikisha wadau wa sekta ili kuweka mikakati ya namna ya kuisaidia sekta isiathirike zaidi,” alisema Dk. Kigwangalla.
BAJETI YAPUNGUA
Katika mwaka wa fedha 2020/21, wizara hiyo iliomba kuidhinishiwa zaidi ya Sh bilioni 114.593.
Kati ya fedha hizo, zaidi ya Sh bilioni 69.573 ni kwa matumizi ya kawaida na Sh bilioni 45 miradi ya maendeleo.
Katika mwaka wa fedha 2019/2020, wizara iliidhinishiwa Sh bilioni 120.202 kwa matumizi ya kawaida na miradi ya maendeleo, hivyo bajeti ya wizara hiyo imepungua kwa Sh bilioni 6.
YAPOKEA ASILIMIA 51
Hadi Machi 2020, wizara ilikuwa imepokea zaidi ya Sh bilioni 61.445 sawa na asilimia 51 ya bajeti iliyoidhinishwa na Bunge mwaka jana.
Kati ya fedha hizo, zaidi ya Sh bilioni 47.655 ni kwa matumizi ya kawaida na Sh bilioni 13.790 miradi ya maendeleo.
CHANGAMOTO
Dk. Kigwangalla alisema baadhi ya changamoto zilizojitokeza katika utekelezaji wa majukumu ya wizara katika kipindi cha mwaka wa fedha 2019/2020, ni pamoja na kuwepo uvamizi wa maeneo yaliyohifadhiwa na shoroba, kuongezeka kwa migongano kati ya binadamu na wanyamapori, uhaba wa watumishi pamoja na wafanyakazi wenye ujuzi na utaalamu katika fani mbalimbali, hususan ukarimu.
Pia wanakabiliwa na changamoto ya kuharibika kwa miundombinu ya barabara kutokana na mvua nyingi zilizonyesha hali iliyosababisha ugumu wa kufikika kwenye baadhi ya maeneo mbalimbali yenye vivutio vya utalii.
Katika kukabiliana na changamoto hizo alisema wizara imeendelea kufanya mapitio ya sera, sheria, kanuni na miongozo mbalimbali na kushirikisha wadau katika kuhifadhi maliasili na malikale na kuboresha miundombinu katika maeneo yaliyohifadhiwa na vivutio vya utalii.
KAMATI YATAKA HATUA KUNUSURU UTALII
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii, imeishauri Serikali kuchukua hatua za ziada ili kuvutia watalii kutoka nje kwa kupunguza tozo zinazoathiri sekta ya utalii ikiwemo landing fees kwa mashirika ya ndege yanayotua nchini.
Pia imeishauri Serikali kupunguza tozo katika hifadhi, kutoa masharti nafuu ya maombi ya viza, na kuondoa kwa muda kodi ya ongezeko la thamani (VAT) katika sekta hiyo.
Akiwasilisha maoni, Mwenyekiti wa kamati hiyo, Kemirembe Lwota, alisema sekta ya utalii imekuwa ikichangia wastani wa asilimia 17 ya pato la taifa na asilimia 25 ya fedha za kigeni, hivyo wanashauri wizara kuandaa mkakati madhubuti wa makusanyo ambao utaakisi hali iliyopo hivi sasa.
”Kwa hali hiyo, makusanyo yatokanayo na sekta hii yanatarajiwa kushuka kwa kuwa kwa sasa nchi haipokei idadi kubwa ya watalii kutoka nje ya nchi kama ilivyokuwa hapo awali.
“Hivyo basi, kamati inashauri kwamba wizara iandae mkakati madhubuti wa makusanyo ambao utaakisi hali iliyopo hivi sasa.
“Mkakati huo uende sambamba na kutoa ahueni kwa wafanyabiashara mbalimbali waliowekeza katika sekta ya utalii, ambao wamekuwa msaada katika kulisaidia taifa kukusanya mapato yake katika sekta hii,” alisema Lwota.
Aidha, kamati imeshauri kupunguza tozo katika hifadhi, kutoa masharti nafuu ya maombi ya viza, na kuondoa kwa muda kodi ya ongezeko la thamani (VAT) katika sekta hii.
“Vilevile, Wizara inaweza ikarejesha kwa muda utaratibu wa single entry katika hifadhi zetu,” alisema Lwota.
Alisema vilevile kamati inashauri wizara kwa kushirikiana na mashirika ya uhifadhi yakiwemo NCAA, Tanapa pamoja na Tawa wawe na mpango wa dharura endapo litatokea jambo lolote duniani ambalo litaathiri sekta ya utalii.
Lwota alisema mpango huo unaweza kuanzisha mfuko maalumu wa kuwezesha uhifadhi kwa lengo la kuwa na akiba ya fedha katika nyakati za uhaba wa mapato.
CHANZO MTANZANIA DIGITAL
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.