MKUU wa wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma Dr.Julius Ningu,ameupongeza mtandao wa vikundi vya wakulima Tanzania(MVIWATA)mkoani humo kutokana na kufanya ufuatiliaji katika sekta ya kilimo na kubaini changamoto ya baadhi ya miradi ya skimu za umwagiliaji kujengwa chini ya kiwango na mingine kushindwa kukamilika kwa wakati na kutoa tija kwa wakulima wa maeneo hayo.
Ningu alitoa pongezi hizo hivi karibuni katika ukumbi wa ofisi ya mkuu wa wilaya ya Namtumbo mara baada ya kupokea taarifa ya mrejesho wa ufuatiliaji wa raslimali za umma kupitia mradi wa utawala Bora unaotekelezwa na mtandao huo katika kata ya Ligera,Limamu na Kitanda wilayani humo kutoka kwa mratibu wa Mviwata wa mkoa wa Ruvuma Laika Haji.
Alisema kuwa Mviwata ni mdau mkubwa wa maendeleo katika kuisaidia serikali kwenye kutoa elimu kwa wakulima hivyo ameushauri mtandao huo kuendelea kupanua wigo wa utendaji wao wa kazi hususani katika kufanya tathmini wakati wa mavuno ya wakulima na kuzingatia takwimu pindi wanapofanya ufuatiliaji wa miradi mbalimbali badala ya kutoa elimu peke yake.
Kufuatia hali hiyo mkuu huyo wa wilaya ya Namtumbo Ningu amewaagiza wataalam wa idara ya kilimo wilayani humo kuzungukia miradi hiyo ya skimu za umwagiliaji zenye changamoto hizo ambazo ni za Namahoka Mwangaza na Mtakuja zilizopo katika kata hizo.
Aidha amewataka madiwani na wataalam wilayani humo kuhakikisha wanasimamia kikamilifu miradi ya maendeleo inayotekelezwa kwenye kata zao kupitia ufadhili kwa lengo la kuwafanya wahisani waendelee kusaidia miradi hiyo ili iweze kuleta manufaa kwa wananchi na kwamba ameuomba mtandao huo kuangalia uwezekano wa kushawishi wadau mbalimbali wa kilimo kusaidia miradi hiyo ili iweze kukamilika.
“Mara nyingi miradi mingi ya kilimo cha umwagiliaji inashindwa kukamilika kwa wakati na kutoa tija kwa wakulima kutokana na ukosefu wa raslimali fedha na uchelewaji wa mapokezi wa fedha hizo za kuendeshea miradi hiyo”Alisema Ningu
Awali akizungumza katika kikao hicho ambacho kilishirikisha baadhi ya madiwani,wataalam pamoja na watumishi wa Halmashauri ya wilaya ya Namtumbo, mratibu wa Mviwata wa mkoa wa Ruvuma Laika Haji alisema kuwa mtandao huo tangu uanze kutoa elimu kwa wakulima na kufanya ufuatiliaji wa raslimali za umma katika sekta ya kilimo kupitia mradi wa utawala Bora umejaribu kuchochea kasi ya maendeleo kwa wakulima.
Naye katibu tawala wa wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma Aden Nchimbi,akizungumza katika kikao hicho alisema kuwa wilaya hiyo imejipanga katika kuhakikisha inaboresha baadhi ya miradi ya kilimo cha umwagiliaji ili iweze kuleta tija na kuwainua wakulima kiuchumi.
Mkurugenzi mtendaji wa Halashauri hiyo Chiliku Chilumba akiongea kwenye kikao hicho alisema kuwa amepokea maagizo yote yaliyotolewa na mkuu wa wilaya ya Namtumbo Dr.Julius Ning una kuyafanyia kazi ikiwa pamoja na kuunda timu ya wataalam watakaozungukia miradi hiyo ya skimu za umwagiliaji kwa lengo la kuangalia changamoto mbalimbali.
Kwa upande wake mwezeshaji katika kikao hicho Mnung’a Shaibu Mnung’a alisema kuwa tangu Mviwata ianze shughuli ya ufuatiliaji wa miradi hiyo imeweza kubaini changamoto mbalimbali ikiwemo ya ukosefu wa uwazi na ushirikishwaji wa wananchi pindi miradi ya maendeleo inapotekelezwa kwenye maeneo yao.
Mnung’a ameishauri Halmashauri ya wilaya ya Namtumbo kuacha tabia ya kuanzisha miradi mipya ya maendeleo kila mwaka na kuacha kukamilisha miradi viporo ambayo imeshindwa kukamilika kwa muda mrefu na kutoa tija kwa wananchi.
Imeandikwa na Julius Konala
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.