Mkuu wa Wilaya ya Songea, Mheshimiwa Kapenjama Ndile, amewahimiza wananchi wa Halmashauri ya Wilaya ya Madaba kuanza kulima zao la ngano, akisisitiza kuwa soko tayari lipo kupitia kampuni ya bia ya Serengeti.
Akizungumza na wananchi, Ndile alisema ofisi yake imefanya mazungumzo na kampuni hiyo, ambayo imekubali kununua ngano mara baada ya mavuno.
Aliahidi kutoa mbegu bure kwa wakulima wenye mashamba ya hekari moja au zaidi, huku akisisitiza juhudi za kuwawezesha kupata mbolea.
“Mwaka huu nimebuni mpango huu, na nyie mnatakiwa kuniunga mkono. Tutawapeni mbegu bure, na kampuni ya Serengeti tayari imekubali kununua mazao yenu,” alisema.
Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Mheshimiwa Teofanes Mlelwa, amempongeza Mkuu wa Wilaya kwa juhudi zake, akibainisha kuwa miaka 30 iliyopita wananchi wa eneo hilo walikuwa wakilima ngano lakini walikata tamaa kutokana na kukosekana kwa soko.
“Kwa maelekezo mazuri ya Mkuu wa Wilaya, kwamba ataleta mbegu na wanunuzi wa zao la ngano, tunaomba mpango huu utekelezwe haraka ili wananchi waweze kulima kwa wakati,” alisema Mlelwa.
Wananchi wamehimizwa kuchangamkia fursa hiyo ili kuboresha maisha yao na kuchangia maendeleo ya kilimo katika wilaya hiyo.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.