MKUU wa wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma Julius Mtatiro,amekabidhi pikipiki 62 kwa maafisa ugani na pikipiki 2 kwa maafisa ushirika wa Halmashauri ya Tunduru kwa lengo la kuwarahisishia kazi ya kuwafikia na kuwahudumia wakulima katika maeneo yao.
Akizungumza na wataalam hao alisema,pikipiki hizo zimetolewa na Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan, kama mpango wake wa kuboresha sekta ya kilimo ili iweze kuleta tija kwa wakulima na Taifa.
Alisema,wakulima wa wilaya hiyo kwa muda mrefu wameshindwa kufikia malengo ya uzalishaji kwa kuwa wanaendelea na kilimo cha mazoea kutokana na kukosa wataalam wa kuwapa elimu,hivyo matumaini yake kuwa pikipiki hizo zitakwenda kuongeza uzalishaji na kukuza uchumi kupitia sekta ya kilimo.
“ndugu zangu maafisa ugani,serikali imetoa malengo ya kuzalisha tani laki nne za korosho nchi nzima, na sisi wilaya yetu imepewa lengo la kuzalisha tani elfu thelathini na tano katika msimu wa kilimo 2022/2023,hivyo kupitia kwenu lazima tufikie malengo hayo”alisema.
Mkuu huyo wa wilaya,ameagiza pikipiki hizo ziwasaidie maafisa ugani kuwatembelea wakulima kwa wakati kwa ajili ya kuwapa huduma za ugani ili waachane na kilimo cha mazoea.
Mtatiro alisema, uzalishaji ukioongezeka upo uwezekano mkubwa pia mapato ya Serikali kupitia Halmashauri ya wilaya yataongezeka, ambapo ametoa siku kumi na nne kwa vongozi wa Halmashauri hiyo kupeleka mpango kazi ofisini kwake namna maafisa ugani hao watakavyoweza kumudu gharama za uendeshaji wa pikipiki hizo.
Amewakumbusha maafisa ugani kwamba, wana wajibu wa kuhakikisha pikipiki walizopewa zinatumika kwa shughuli iliyokusudiwa ikiwani pamoja na kuwahudumia wakulima kwani itasaidia wakulima kutokuwa na manung’uniko ya kutofikiwa na wataalam hao.
Amewaomba kutomwangusha Rais Samia Hassan kutokana na kazi kubwa ya kusaidia na kuinua sekta ya kilimo hapa nchini,kwa hiyo ni mategemeo ya serikali kuwa, pikipiki hizo zitatumia kuleta mapinduzi makubwa ya kilimo katika wilaya hiyo.
Hata hivyo alisisitiza kuwa,afisa ugani yeyote atakayebainika kugeuza matumizi ya pikipiki hizo kuwa bodaboda atanyang’anywa ikiwa ni pamoja na kuchukuliwa hatua za kinidhamu.
Mtatiro ambaye ni mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama wa wilaya hiyo, amewaasa maafisa ugani hao kuzingatia sheria za usalama barabarani ili kuepuka ajali zisizo za lazima na kuepuka kuwabeba watu wasiowafahamu wanaoweza kuwateka na kuwapora pikipiki.
“mjihadhari sana kuwabeba watu wa onyo ovyo,kuna wengine sio waaminifu watawanyonga na kuwapokonya pikipiki hizi”alisema Mtatiro.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya Tunduru Jonathan Haule, amewataka kuzingatia na kufuata sheria za barabarani na kuwa na matumizi sahihi ya kwenda kuwasaidia wakulima walime kilimo chenye tija.
Akizungumza kwa niaba ya wenzake Afisa kilimo wa kata ya Tinginya Jamal Said,amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwapatia usafiri huo kwani kwa muda mrefu wamekuwa wakipata shida kuwatembelea wakulima.
Jamal alisema, pikipiki hizo walizopewa na Serikali watakwenda kufanya mapinduzi makubwa ya kilimo na kuongeza uzalishaji wa mazao kwa wakulima wa wilaya hiyo ya Tunduru.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.