Halmashauri za Manispaa ya Songea na Halmashauri ya Songea mkoani Ruvuma zimepata hati safi kutokana na ukaguzi wa Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG) uliofanyika kuishia Juni 30 mwaka huu.
Akizungumza kwa nyakati tofauti kwenye vikao maalum vya kujadili taarifa ya CAG katika mabaraza ya madiwani katika Halmashauri hizo,Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge amezipongeza Halmashauri hizo kwa kufanikiwa kupata hati safi.
Akizungumza katika Halmashauri ya Manispaa ya Songea Ibuge ameipongeza Halmashauri hiyo kwa kuweza kukusanya mapato ya ndani kwa asilimia 94.67 ya lengo la kukusanya mapato Zaidi ya shilingi bilioni 3.97 ambapo wameweza kukusanya Zaidi ya shilingi bilioni 3.76 katika kipindi cha mwaka wa fedha 2020/2021.
“Nitumie nafasi hii kuelezea masikitiko yangu kwa Halmashauri ya Manispaa ya Songea kwa kuchangia asilimia 43.06 tu kwenye mfuko wa wanawake,vijana na watu wenye ulemavu ambapo mmeweza kuchangia shilingi 138,100,00 tu kati ya shilingi 320,715,281 ambazo mlipaswa kuchangia’’,alisisitiza Ibuge.
Akizungumza katika kikao maalum cha CAG katika Halmashauri ya Wilaya ya Songea,Mkuu wa Mkoa ameipongeza Halmashauri hiyo kwa kukusanya mapato ya ndani kwa asilimia 79 katika mwaka wa fedha unaoishia Juni 30 mwaka huu.
Amesema katika kipindi hicho Halmashauri hiyo iliweza kukusanya kiasi cha Zaidi ya shilingi bilioni 1.32 kati ya lengo la kukusanya Zaidi ya shilingi bilioni 1.67 katika mwaka wa fedha 2020/2021.
Hata hivyo amesisitiza kuwa makusanyo hayo bado ni chini ukilinganisha na kiwango kilichowekwa cha kukusanya angalau asilimia 81 ya lengo.
RC Ibuge pia amesikitishwa na Halmashauri hiyo kuchangia asilimia 50.3 tu ya mfuko wa wanawake,vijana na wenye ulemavu ambapo wameweza kuchangia Zaidi ya shilingi milioni 66 tu kati ya Zaidi ya milioni 132 ambazo zilipaswa kuchangiwa katika kipindi hicho.
Katika kikao hicho Mkuu wa Mkoa ameagiza Halmashauri zote kuhakikisha hoja zote zilizosalia zifungwe na kuzuia kujirudia kwa hoja na kwamba wakuu wa Idara washiriki kikamilifu kuandaa majibu ya hoja na utekelezaji wa mapendekezo ya CAG.
Mkuu wa Mkoa pia ameagiza Halmashauri zote zichukue mapema hatua za kinidhamu kwa watumishi wanaozalisha hoja,pia ameagiza kudhibiti upotevu wa mapato katika Halmashauri na kwamba Halmashauri ziendelee kulipa madeni mbalimbali ya wazabuni kwa wakati ili kujiendesha kwa tija.
RC Ibuge pia ameziagiza Halmashauri kusimamia kikamilifu mfuko wa Bima ya Afya na Bima ya Afya iliyoboreshwa ili kila mwananchi aweze kujiunga ikiwa ni Pamoja na kufuatilia malipo yake kwenye vituo vya afya na zahanati.
Mstahiki Meya wa Manispaa ya Songea Mheshimiwa Michael Mbano na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Songea Mheshimiwa Menace Komba wameahidi maagizo yote yaliyotolewa na Mkuu wa Mkoa kuyafanyia kazi kwa haraka.
Imeandikwa na Albano Midelo
Afisa Habari Kitengo cha Mawasiliano Serikalini,Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma
Juni 25,2022
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.