MKUU wa Mkoa wa Ruvuma Christina Mndeme ameipongeza Halmashauri ya Mji wa Mbinga kwa kuendelea kupata hati safi tangu kuanzishwa kwa Halmashauri hiyo miaka mitatu iliyopita.
Mndeme ametoa pongezi hizo wakati anafungua kikao maalum cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri hiyo cha kujadili taarifa za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka wa fedha za 2018/2019 mjini Mbinga.
Taarifa ya CAG inayoishia Juni 30,2019 imeonesha kuwa Halmashauri ya Mji wa Mbinga imepata hati safi na kwamba mwenendo wa hati za ukaguzi katika Halmashauri hiyo imekuwa ni wa kuridhisha kwa miaka mitatu mfululizo kuanzia mwaka wa fedha wa 2016/2017 hadi 2018/2019.
“Napenda niwakumbushe kuwa kupata hati safi kwa miaka mitatu mfululizo sio jambo dogo,hongereni sana,hivyo naomba niwape shime kwamba kupatikana kwa hati hizo kuwafanye muongeze bidii zaidi’’,alisisitiza.
Mndeme pia amewapongeza madiwani na watalaam wa Halmashauri hiyo kwa kuweza kuchangia kwa asilimia 100 mfuko wa wanawake,vijana na wenye ulemavu ambao wamechangia zaidi ya shilingi milioni 112.
Katika kikao hicho,Mndeme ametoa maagizo kwa uongozi wa Halmashauri hiyo ambayo ni kuzuia kuwepo kwa hoja zinazojirudia mwaka hadi mwaka,wakuu wa Idara kushiriki ipasavyo katika kuandaa majibu ya hoja,utekelezaji wa mapendekezo ya CAG na kuchukua hatua kwa watumishi wanaozalisha hoja.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Mbinga Grace Quentin,akizungumza katika kikao hicho,amesema makusanyo ya mapato ya ndani katika mwaka wa fedha wa 2018/2019.makisio yalikuwa ni kukusanya zaidi ya bilioni 1.4 hata hivyo makusanyo halisi yalikuwa ni zaidi ya bilioni 1.5 sawa na asilimia 107.15.
Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Mbinga David Mapunda ameahidi kusimamia utekelezaji wa maagizo yote aliyoyatoa Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma ili kuhakikisha kuwa Halmashauri hiyo inaendelea kuwa mfano kwa Halmashauri nyingine.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Mbinga Cosmas Nsenye ameyataja mafanikio yaliyopatikana katika wilaya hiyo ikiwemo kupata hati safi na kukamilisha miradi kwa wakati,yametokana na uwepo wa ushirikiano na mshikamano baina ya madiwani na watalaam.
Halmashauri ya Mji wa Mbinga ni miongoni mwa Halmashauri sita kati ya nane zilizopo katika Mkoa wa Ruvuma zilizopata hati ya safi kwenye ukaguzi wa CAG wa mwaka wa fedha 2018/2019.
IMEANDIKWA NA ALBANO MIDELO
AFISA HABARI WA MKOA WA RUVUMA
MEI 28,2020
MBINGA
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.