Halmashauri ya wilaya ya Songea Mkoani Ruvuma imeingia mkataba na kampuni ya West Food Comp LTD ya kutoka Makambako Mkoani Njombe kwa ajili ya kukusanya ushuru wa mazao.
Makubaliano ya mkataba huo yamefanyika katika Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo kwa kuwekeana saini baina ya Mkurugenzi wa Kampuni na Uongozi wa Halmashauri.
Akisaini mkataba huo Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Tanu Kameka ametoa wito kwa Kampuni hiyo kufanya kazi waliyoomba kwa ufanisi kwasababu Serikali inategemea mapato kwa ajili ya kutekeleza majukumu yake.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa kampuni hiyo Godwin Chengula ameahidi kufanyakazi kwa ufanisi na kwamba ana uzoefu katika kazi ya ukusanyaji ushuru ambayo ameifanya katika maeneo ya Wilaya za Ulanga ,Ifakara ,Makambako na Manispaa ya Songea
Naye Mweka Hazina wa Halmashauri hiyo Rajabu Lingoni amesema katika kuboresha ukusanyaji wa mapato vikao vya kisheria vilikubaliana kumpata mzabuni atakayefanya kazi ya ukusanyaji wa ushuru wa mazao badala ya kuendelea kuwatumia mawakala.
“Maamuzi hayo yamefikia baada ya kubaini udanganyifu mkubwa katika ukusanyaji wa ushuru,unaofanywa na baadhi watendaji wa Kata kupitia mawakala wao kitendo ambacho kilikuwa kinakwamisha jitihada za Halmashauri katika kutekeleza majukumu yake’’,alisisitiza.
Lingoni amesema jumla ya vizuio 15 vimeanishwa na vimekabidhiwa kwa mzabuni ambavyo vitatumika katika kukusanya ushuru wa mazao katika kipindi cha mwaka mmoja kuanzia Machi 2021hadi Machi 2022.
Hata hivyo amesema mzabuni anatakiwa kukusanya ushuru kwa kuzingatia taratibu,kanuni na sheria za ukusanyaji wa mapato zilizowekwa na Serikali.
Kwa upande wake Mhasibu wa Mapato wa Halmashauri hiyo Noel Chengula ameutaja utaratibu wa kutoa zabuni katika kazi ya ukusanyaji ushuru ni kitendo kitakachoongeza ufanisi na kuondoa usumbufu na gharama za kuwalipa mawakala ambao awali walikabidhiwa jukumu hilo.
Chengula amesema jambo hilo litapunguza changamoto ya madeni kwa baadhi ya Watendaji wa Kata,Vijiji na mawakala na kwamba gharama za ufuatiliaji,na fedha za makusanyo zitafikishwa benki kwa wakati.
Imeandikwa na Albano Midelo
Afisa Habari Mkoa wa Ruvuma
Machi 15,2021
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.