HALMASHAURI ya Wilaya ya Songea mkoani Ruvuma imepata hati yenye mashaka kwa ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka wa fedha 2018/2019.
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Christina Mndeme akifungua kikao Maalum cha Baraza la madiwani la Halmashauri hiyo cha kujadili hoja na mapendekezo ya CAG kilichofanyika Ikulu ndogo ya Songea,amesema ameumizwa na kusitikishwa na hati hiyo ambayo ni ishara kuwa hakuna ushirikiano kati ya madiwani na wataalam.
“Nachukua fursa hii kwa namna ya pekee kutoa masikitiko yangu hati yenye mashaka imeniumiza na kunisikitisha sana’’,alisema Mndeme.
Kutokana na hati yenye mashaka Mndeme amewaagiza madiwani na watalaam wa Halmashauri ya Songea kuongeza nguvu katika utendaji kazi na kuimarisha mshikamano na umoja ili hali hiyo isijitokeza tena.
Hata hivyo Mkuu wa Mkoa amesema,licha ya kupata hati yenye mashaka kwa mwaka 2018/2019,mwenendo wa hati za ukaguzi kwa miaka minne katika halmashauri hiyo unaonesha kuwa mwaka 2015/2016 Halmashauri ilipata hati yenye mashaka,2016/2017, hati inayoridhisha, 2017/2018 hati inayoridhisha na 2018/2019 hati yenye mashaka.
Amesema ndani ya miaka minne Halmashauri hiyo imepata hati mbili zenye mashaka,hali ambayo amesema ni ishara tosha ya kukosekana kwa uwajibikaji ambapo ameagiza kila mtumishi kutimiza wajibu wake pamoja na kusimamia matumiz sahihi ya fedha za umma.
Katika hatua nyingine Mkuu wa Mkoa ametoa siku saba kwa Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo kuwalipa madiwani posho zao zote wanazodai ambazo ni zaidi ya shilingi milioni 36.
Mndeme pia ameagiza kufunguliwa ofisi na kuwepo mtaalam katika shamba la kahawa la AVIV lililopo katika kijiji cha Lipokela ambalo ni chanzo kikubwa cha mapato ya ndani katika Halmashauri hiyo.
“Naagiza mtaalam huyo kukusanya takwimu za uzalishaji na mauzo ya kahawa katika shamba hilo ili serikali iweze kupata mapato sahihi,pia kupitia shamba hili,amashisheni wakulima kulima kahawa’’,alisisitiza Mndeme.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Rajabu Mtiula amemuomba radhi Mkuu wa Mkoa kutokana na Halmashauri hiyo kupata hati yenye mashaka ambapo amemthibitishia hali hiyo haitarudia tena na kwamba maagizo yote aliyotatoa watayafanyia kazi.
Halmashauri ya Wilaya ya Songea na Halmashauri ya Manispaa ya Songea ni miongoni mwa Halmashauri mbili kati ya nane zilizopo mkoani Ruvuma ambazo zimepata hati zenye mashaka katika ukaguzi wa CAG wa mwaka wa fedha 2018/2019.
Imeandikwa na Albano Midelo
Afisa Habari wa Mkoa wa Ruvuma
Juni 6,2020
Songea
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.