Katika anga ya majonzi , taifa linamsindikiza mmoja wa wazee wake mashuhuri, Hayati Alhaj Mohamed Mustafa Songambele.
Katika tukio hilo la kihistoria lililofanyika Mahenge mjini Songea mkoani Ruvuma, Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dkt. Emmanuel John Nchimbi, amefichua urithi mkubwa alioacha Mzee Songambele,kitabu cha kihistoria kiitwacho “Safari ya Karne”, ambacho kimetajwa kuwa hazina ya kipekee katika kuelezea historia ya uhuru na maendeleo ya Tanzania.
Akitoa salamu za pole kwa niaba ya CCM na Serikali, Balozi Nchimbi alisema Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameagiza shughuli zote za msiba huo kugharamiwa na Serikali, ikiwa ni heshima kwa mchango mkubwa wa Hayati Songambele katika ujenzi wa taifa.
Alisisitiza kuwa CCM itasimamia mchakato wa uchapaji wa kitabu hicho ili kizazi cha sasa na kijacho kipate maarifa ya kina kuhusu harakati za ukombozi na msingi wa Tanzania ya leo.
Kitabu cha Safari ya Karne kinaelezea kwa kina maisha na mchango wa Mzee Songambele, kuanzia mapambano ya uhuru, uhusiano wake wa karibu na Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere, hadi kuundwa kwa Tanzania na hatimaye kuzaliwa kwa CCM.
Balozi Nchimbi alieleza kuwa awali kitabu hicho kilipendekezwa kiitwe Swahiba wa Nyerere, lakini baadaye Mzee Songambele alikibadilisha jina baada ya kutambua kuwa anakaribia kutimiza miaka 100 ya maisha yenye historia nzito.
“Alinikabidhi niandike dibaji ya kitabu hicho na nilifanya hivyo kwa moyo wote,” alisema Balozi Nchimbi kwa hisia.
Alimwelezea Hayati Songambele kama kiongozi mwenye maono, aliyetoa mchango usio na kifani katika siasa na maendeleo ya taifa, akiwa chimbuko lake ni Mkoa wa Ruvuma.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: KERO PIGA 0800110174
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.