Katika kilele cha maadhimisho ya Siku ya Homa ya Ini Duniani, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeweka wazi mafanikio makubwa katika mapambano dhidi ya ugonjwa huu hatari unaoathiri mamilioni ya watu duniani. Akizungumza Julai 28, 2025 kupitia vyombo vya habari mkoani Ruvuma, Waziri wa Afya, Mhe. Jenista Mhagama, amesema Tanzania imepiga hatua kubwa katika upimaji, tiba, na utoaji wa chanjo ya Homa ya Ini – hatua zinazoweka msingi wa kutokomeza kabisa ugonjwa huo ifikapo mwaka 2030.
Kwa mujibu wa utafiti wa Viashiria na Matokeo ya UKIMWI Tanzania (THIS 2022/2023), kiwango cha maambukizi ya Homa ya Ini inayosababishwa na virusi aina ya B kimeshuka kutoka asilimia 4 (2016/17) hadi asilimia 3.5, huku maambukizi ya virusi vya aina C yakiwa yameshuka kutoka asilimia moja hadi 0.2.
“Takwimu hizi ni ushahidi wa mafanikio ya jitihada za Serikali kwa kushirikiana na wadau wa afya katika kutoa elimu, huduma za kinga na tiba. Tumejipanga kuhakikisha tunafikia lengo la kidunia la kutokomeza Homa ya Ini ifikapo mwaka 2030,” alisema Mhe. Mhagama.
Huduma za upimaji na matibabu ya Homa ya Ini kwa sasa zinapatikana katika Hospitali zote za Rufaa za Mikoa, Kanda na Hospitali ya Taifa ya Muhimbili. Vituo vya afya vya Wilaya, Zahanati na Vituo vya Afya pia vinaendelea kutoa huduma za upimaji na kutoa rufaa, huku Serikali ikifanya maandalizi ya kuviwezesha vituo hivyo kutoa huduma za moja kwa moja za matibabu ya Homa ya Ini.
Aidha, Waziri Mhagama alibainisha kuwa huduma ya chanjo ya Homa ya Ini aina ya B inatolewa bure kwa watoto wachanga waliotangazwa tangu mwaka 2002 kupitia chanjo ya mchanganyiko (Pentavalent), huku watu wazima wakihimizwa kupata chanjo kwa kuchangia gharama ndogo katika vituo vya afya.
Homa ya Ini ni ugonjwa unaosababishwa na virusi vya aina tano – A, B, C, D na E – ambapo aina ya B ndio inayoongoza kwa maambukizi nchini. Virusi vya aina A na E huambukizwa kupitia ulaji wa chakula au unywaji wa maji yaliyochafuliwa, huku virusi vya aina B, C na D huenea kwa njia zinazofanana na maambukizi ya VVU – zikiwemo kuongezewa damu iliyoambukizwa, kujamiiana bila kinga, matumizi ya sindano zisizo salama, kujichoma kwa vitu vyenye ncha kali, au kuambukizwa kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto wakati wa kujifungua.
“Ni muhimu kwa kila mwananchi kuchukua tahadhari kwa kujikinga na kujitokeza kupima afya zao. Tunawahamasisha Watanzania kujitokeza kwa wingi kupata chanjo na huduma za upimaji zilizopo karibu yao,” alisisitiza Waziri Mhagama.
Katika hotuba yake, Waziri Mhagama alitoa wito kwa wananchi kote nchini kuwekeza katika kinga dhidi ya Homa ya Ini, hasa kwa kupata chanjo, kula vyakula safi na salama, kutumia maji yaliyochemshwa au yaliyotibiwa, na kuepuka tabia hatarishi kama vile kujamiiana bila kinga au kutumia vifaa vyenye ncha kali kwa pamoja.
“Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi thabiti wa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan imejizatiti kuhakikisha huduma za afya zinamfikia kila Mtanzania. Mapambano dhidi ya Homa ya Ini ni jukumu letu sote,” alisema kwa msisitizo.
Pamoja na mafanikio yanayoonekana kwa kupungua kwa maambukizi ya Homa ya Ini nchini, bado kuna safari ndefu kufikia kutokomeza ugonjwa huu kabisa. Ni jukumu la kila mmoja kuendelea kushiriki kikamilifu katika juhudi za kinga, upimaji na matibabu.
Kwa kushirikiana – Serikali, jamii, na wadau wa maendeleo – Tanzania inaweza kuwa mfano bora wa mafanikio ya afya ya umma katika bara la Afrika. Vita dhidi ya Homa ya Ini siyo ndoto, bali ni lengo linalowezekana kwa mshikamano na hatua madhubuti.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: KERO PIGA 0800110174
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.