Waziri wa Afya, Mhe. Jenista Mhagama, amesema viashiria vya ushamili wa homa ya ini vinaonyesha kuwa umeshuka nchini kwa takwimu za utafiti wa homa ya UKIMWI za mwaka 2022/23 ukilinganisha na takwimu za mwaka 2016/17.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Afya, Mhe. Jenista Mhagama, wakati akitoa tamko la wizara katika maadhimisho ya siku ya homa ya ini duniani, ambapo ametoa tamko hilo mkoani Ruvuma.
“Kulingana na takwimu za utafiti wa homa ya UKIMWI kwa mwaka 2022/23 ni asilimia 3.5 kwa homa ya ini inayosababishwa na virusi vya aina ya B, na asilimia 0.2 inavyosababishwa na aina ya C, viashiria vyote vinaonyesha ushamili huo umeshuka kutoka takwimu za utafiti wa hali ya UKIMWI kwa mwaka 2016/17 ambapo ilikuwa ni asilimia 4.0 kwa homa ya ini uambukizo wa virusi vya aina ya B na asilimia 1 inayoambukizwa kwa virusi vya aina ya C,” alisema Mhagama.
Chanjo ya homa ya ini aina ya B hutolewa bila malipo kwa watoto wachanga, huku watu wazima wakichangia kiasi kidogo, hivyo amewataka wananchi kujitokeza kupima viashiria vya ugonjwa ya homa ya ini katika vituo vya kutolea huduma za afya.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Kanali Ahmed Abbas Ahmed, amesema kuwa takwimu za kitaifa za mwaka 2022/2023 zinaonyesha kuwa asilimia 2.0 ya watu wenye umri wa kuanzia miaka 15 wameambukizwa virusi vya homa ya ini, sawa na watu wawili kati ya kila watu 100.
Amebainisha kuwa mkoa wa Ruvuma una zaidi ya watu 24,000 waliothibitishwa kuwa na homa ya ini, ambapo wanaume ni takribani 17,000 na wanawake 7,000.
Maadhimisho ya Siku ya Homa ya Ini Duniani hufanyika kila mwaka tarehe 28 Julai, yakilenga kuongeza uelewa kuhusu ugonjwa huu hatari na kuchochea hatua za kudhibiti maambukizi. Kwa mwaka 2025, kauli mbiu ni: "Ondoa Vikwazo, Tokomeza Homa ya Ini", ikisisitiza umuhimu wa kuondoa changamoto zinazozuia watu kupata elimu sahihi, huduma za afya, na chanjo dhidi ya ugonjwa huo.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: KERO PIGA 0800110174
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.