Hospitali ya Rufaa ya Misheni ya Mtakatifu Joseph Peramiho iliyopo Wilayani Songea, Mkoani Ruvuma imezindua Mashine ya kutolea huduma ya mionzi (CT-Scan) kwa ajili ya kuboresha huduma zinazotolewa katika hospitali hiyo.
Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo Dr. Adeodatus Haule wakati akitoa taarifa ya hospitali hiyo amesema hospitali hiyo iliibua mradi wa kununua na kufunga mashine ya CT-Scan ili kuboresha huduma za upimaji wa magonjwa kwa kutumia teknolojia ya kisasa.
"Hospitali ilipokea fedha kutoka kwa wafadhili Wamisionari Wabenedictine wa Mtakatifu Ottilian Ujerumani kiasi cha Milioni 214,288,583 kwa ajili ya ujenzi wa jengo la CT-Scan, baada ya jengo kukamilika wafadhili hao walinunua mashine ya CT-Scan iliyogharimu fedha za kitanzania Shilingi Bilioni 1,550,745,000,"alisema Dr. Haule.
Amebainisha kuwa mradi huo umekamilika na huduma zimeanza kutolewa tangu Septemba 2024, baada ya kukaguliwa na wataalam kutoka Tume ya Mionzi (TAEC), na wagonjwa takribani 70 wamehudumiwa na mashine hiyo.
Hospitali ya Peramiho iliteuliwa kuwa hospitali teule ya Wilaya ya Songea mnamo Juni 25, 2010 na mwaka 2011 Wizara ya Afya ilipandisha hadhi ya huduma ya hospitali hiyo kuwa kati ya hospitali 10 za mashirika ya dini yanayohudumu katika ngazi ya hospitali ya rufaa ngazi ya Mkoa bila kuondoa makubaliano ya awali ya kuhudumia kama hospitali teule ya Wilaya ya Songea.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.