Pichani ni meli ya MV Mbeya II ikiwa imetia nanga katika bandari ya Mbambabay wilayani Nyasa
SERIKALI imenunua meli tatu zinazotoa huduma za abiria na mizigo katika mikoa ya Ruvuma,Mbeya na Njombe kupitia ziwa Nyasa.
Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) inahudumia jumla ya bandari 15 katika ziwa Nyasa ambapo katika Mkoa wa Ruvuma,TPA inahudumia bandari sita ambazo ni Mbambabay,Liuli,Njambe,Lundu,Mkili na Ndumbi,katika Mkoa wa Njombe TPA pia inahudumia bandari sita ambazo ni Lumbila, Ifungu, Nsisi, Makonde,Lupingu na Manda na katika Mkoa wa Mbeya TPA inahudumia bandari tatu ambazo ni Itungi,Kiwira na Matema.
Baadhi ya bandari TPA imeweka miundombinu ya kisasa,pia kuna bandari ambazo zinaendelea kuwekwa miundombinu kwa ajili ya utoaji huduma bora na za kisasa.
Kila bandari inahitaji kuwa na magati,maghala,yadi za kutunzia mitambo na mizigo na uwepo wa nyumba za kuishi wafanyakazi,sanjari na kuweka mifumo ya zimamoto,majisafi,maji taka na mifumo ya TEHAMA ili kufanyakazi kwa ufanisi na tija kulingana na maelekezo ya serikali.
Ili kuboresha huduma katika bandari zote za ziwa Nyasa,TPA inatekeleza mpango kabambe unaoanza mwaka 2021/2022 na unaotarajia kukamilika katika kipindi cha mwaka 2028/2029.
Mpango huo kabambe utaongeza shehena ya mizigo katika ziwa Nyasa kutoka tani zaidi ya 11,000 hadi kufikia shehena ya mizigo zaidi ya tani 100,000,lengo hili linachochewa na mipango mizuri ya serikali ikiwemo kukamilika kwa ujenzi wa barabara ya lami toka Mbinga hadi Mbambabay.
kutokana na kukamilika kwa lami ya Mbinga hadi Mbambabay na kuanza kutoa huduma za meli katika ziwa Nyasa kunafufua uchumi wa mji wa Mbambabay wilaya ya Nyasa hivyo kuunganisha Tanzania kupitia ushoroba wa Mtwara na nchi za Malawi,Msumbiji , Zimbabwe na Zambia.
Hakuna ubishi Mji wa Mbambabay utafufuka kwa kasi kutokana na kukamilika kwa mtandao wa barabara ya lami kutoka Mbinga hadi Mbambabay na serikali kununua meli tatu mpya kati ya hizo meli mbili za MV Njombe na MV Ruvuma ni za mizigo na meli moja ya MV Mbeya II ni ya abiria.
Kulingana na TPA meli zote tatu zimegharimu zaidi ya shilingi bilioni 20.1 ambazo zimetolewa na serikali kujenga meli kwa kutumia kampuni ya Songoro Marine inayomilikiwa na Mtanzania.
Meli mbili za mizigo MV Njombe na MV Ruvuma kila moja ina uwezo wa kubeba tani 1000 na kwamba kila meli imegharimu shilingi bilioni 5.5 na meli ya abiria ya MV Mbeya II ina uwezo wa kubeba abiria 300 na mizigo tani 200, imegharimu shilingi bilioni 9.1.
Kwa mujibu wa taarifa ya TPA meli ya abiria ya MV Mbeya II imerithi jina la meli ya MV Mbeya I iliyozama eneo la Makonde ziwa Nyasa mwaka 1977.
Hata hivyo meli ya MV Mbeya II baada ya kujengwa iliingizwa majini Septemba 2019
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas anasema wilaya ya Nyasa sasa imefunguka kutokana na kukamilika kwa ujenzi wa barabara ya lami toka Mbinga hadi Mbambabay na kuanza rasmi kwa huduma za meli tatu ndani ya ziwa Nyasa.
Amesema huduma za meli zinaimarishaji bandari katika ziwa Nyasa na kuchochea shughuli za kiuchumi hususani biashara na uwekezaji na sekta ya utalii.
Mkuu wa Mkoa anatoa rai kwa watanzania waliopo ndani na nje ya nchi kufika kuwekeza katika wilaya ya Nyasa ambayo miundombinu yake imeboreshwa ikiwemo barabara ya lami,umeme na usafiri wa majini.
Mhandisi Stella Manyanya ni Mbunge wa Jimbo la Nyasa anasema kuboreshwa kwa barabara na uwepo wa meli mpya kutaongeza idadi ya wageni wanaotembelea wilaya Nyasa ambayo ni kitovu cha utalii katika Mkoa wa Ruvuma.
Imeandikwa na Albano Midelo wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Mkoa wa Ruvuma
Aprili 3,2023
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.