KAMATI ya Siasa ya CCM Mkoa wa Ruvuma ikiongozwa na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa Musa Homera imeendelea na ziara ya kutembelea na kukagua miradi ya maendeleo katika Mkoa wa Ruvuma.
Kamati hiyo imekagua ujenzi wa jengo la upasuaji na ukarabati wa jengo la wagonjwa wa nje (OPD) katika kituo cha afya Kindimbachini kata ya Muungano Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga na kuridhishwa na hatua ya utekelezaji wa mradi huo ambao utawaondolea kero wananchi kusafiri umbali wa zaidi ya kilometa 120 kutafuta huduma ya upasuaji .
Akisoma taarifa ya mradi huo Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga Juma Mnwele amesema mradi wa jengo la upasuaji ulianza mwaka 2016 na kwamba wananchi walihamasika kuchangia ujenzi huo na ambapo gharama za mradi hadi utakapokamilika na vifaa ni zaidi ya milioni 72.
Akizungumzia ukarabati wa jengo la wagonjwa wa nje,Mkurugenzi huyo amesema,ukarabati unaendelea vizuri na kwamba gharama za ukarabati wa jengo hilo ni milioni 34, fedha hizo zinatokana na ruzuku ya afya ya mfuko wa pamoja kwa ajili ya matokeo ya ufanisi.
“Mradi wa jengo la upasuaji upo katika hatua za umaliziaji,pia ukarabati wa jengo la wagonjwa wa nje unaendelea vizuri,mradi huu utanufaisha wananchi wote wa kata za Muungano na maeneo jirani ya kata ya Namswea,Ruanda na Litumbandyosi’’,alisema.
Uchunguzi umebaini kuwa katika kata hizo hakuna kituo cha afya cha serikali hivyo wananchi kwa miaka mingi wanakosa huduma muhimu kama ya upasuaji ambayo sasa wataipata katika kituo cha afya Kindimbachini.
Hata hivyo Mnwele anaitaja changamoto kubwa inayowakabili wananchi wa kata hiyo kuwa ni ubovu wa barabara ambayo kipindi cha masika inaweza kusababisha madhara kwa uhai wa mgonjwa anayehitaji huduma za rufaa katika hospitali kubwa na ukosefu wa huduma nyingine za kijamii kama umeme na maji.
Akizungumza mara baada ya kukagua mradi huo Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa Musa Homera amewapongeza wananchi wa Kindimbachini kwa kusimamia vema mradi huo ambao amesema unakwenda kuondoa kero ya huduma ya upasuaji ambayo wananchi wameipata kwa miaka mingi.
Naye Katibu wa CCM Mkoa wa Ruvuma Nuru Ngeleja amewataka wananchi wa Kindimbachini ili kumtia moyo Rais Dkt.John Magufuli wajitokeze kwa wingi kumchangua Rais,wabunge na madiwani katika uchaguzi mkuu mwaka huu kwa kuwapa kura zote za ndiyo.
Imeadikwa na Albano Midelo
Afisa Habari wa Mkoa wa Ruvuma
Julai mosi,2020
Mbinga
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.