KAMATI ya Siasa ya CCM Mkoa wa Ruvuma imewaagiza watendaji wa serikali wilayani Namtumbo kufanya marekebisho ya mapitio katika hifadhi Jamii za Jumuiya za Mbarang’andu na Kindamba kabla ya Agosti 30 mwaka huu.
Maagizo hayo yametolewa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo Oddo Mwisho wakati anazungumza na wananchi wa kijiji cha Mchomoro wilayani Namtumbo,baada ya kukagua hifadhi ya Jumuiya ya Mbarang’andu ambayo wananchi wamekuwa wanalalamika kutotendewa haki na baadhi ya watendaji wa hifadhi hiyo.
Mwisho amesema utaratibu wa serikali katika hifadhi za jumuiya za kijamii inatakiwa kufanyiwa mapitio na marekebisho kila baada ya miaka kumi ambapo katika hifadhi hizo jambo hilo halijafanyika kwa miaka saba katika hifadhi ya Mbarang’andu na miaka miwili katika hifadhi ya Kindamba hivyo kulenga mgogoro baina ya serikali na wananchi.
Amesema hifadhi za jamii hizo zinazozungukwa na vijiji 15 ni muhimu kwa uhifadhi endelevu kwa watanzania wote kwa kuwa zinahifadhi mazingira na kuepusha nchi yetu kugeuka jangwa na kusababisha ukame.
Hata hivyo Mwisho ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Ruvuma amesema baada ya kupata taarifa kuwa watendaji wa Wizara husika hawajafanya mapitio kulingana na makubaliano na sheria ndipo waliamua kufanya ziara ya ukaguzi wa maeneo hayo na kuamua kutoa maagizo kama chama tawala ambacho kinaongoza serikali.
“Wananchi walioingia kulima kwenye hifadhi wana makosa na watendaji wa serikali walioshindwa kufanya marekebisho ya hifadhi kwa mujibu wa sheria wana makosa kwa sababu hifadhi zilipaswa kufanyiwa mapitio upya kila baada ya miaka kumi kulingana na makubaliano ya serikali na wananchi wenye maeneo ya hifadhi’’,alisisitiza.
Amesisitiza kuwa ifikapo Agosti 30 mwaka huu wamekubaliana na watendaji wa serikali marekebisho ya hifadhi yawe yamefanyika na kwamba wamekubaliana pia viongozi wa Jumuiya hizo ambao wapo madarakani kwa miaka 17 kinyume cha sheria waondolewe na uchaguzi ufanyike wa kuwapata viongozi wengine wapya.
Mwisho amesisitiza kuwa watendaji wa serikali wapite katika vijiji vyote 15 vinavyozunguka hifadhi hizo na kufikia makubaliano mapya ya mapitio ya hifadhi hizo na kuingia makubaliano mapya kuzunguka hifadhi hizo.
Ameagiza wananchi waliovamia hifadhi kwa kulima mpunga ndani ya hifadhi wajitokeze ili watambuliwe na ikiwezekana mazao ambayo wamenyang’anywa na watendaji wa hifadhi yarudishwe kwa wananchi.
Mwenyekiti huyu wa CCM Mkoa wa Ruvuma amesema lengo ni kukomesha uvamizi kwenye maeneo ya hifadhi hizo,hivyo wananchi wasiogope kujitokeza kuhofia kukamatwa kwa sababu Kamati imekubaliana na wahifadhi kuwa waliochukuliwa mazao watambuliwe na kwamba wasirudie tena kulima kwenye hifadhi baada ya kumaliza mgogoro huo.
Mwisho amesisitiza kuwa kinachofanywa na Kamati ya Siasa ya Mkoa ni kutekeleza maagizo ya Rais Dkt John Magufuli ya kwenda kwa wananchi na kuona maeneo yenye mgogoro yakoje jambo ambalo halijafanyika kwenye hifadhi za Mbarang’andu na Kimbanda.
Amesema serikali ikishatekeleza maelekezo ya Julai 12 mwaka huu kuhusu kuwarudishia mazao ya mpunga wananchi ambao walichukuliwa mazao yao baada ya kulima kwenye maeneo ya hifadhi,kamati ya Siasa itarudi tena kwenye eneo la hifadhi na kuwaambia wananchi wasirudie kulima tena hadi hapo mapitio ya hifadhi yatakapofanyika.
Afisa Maliasili wa Halmashauri ya Wilaya Namtumbo Erenest Nombo amesema ni kweli kuna wananchi walivamia na kulima eneo la hifadhi za Mbarang’andu na Kimbanda kinyume cha sheria za uhifadhi ambao baadhi wamekamatwa na kesi zipo mahakamani na mazao yao yamechukuliwa na serikali ambapo hadi sasa kuna magunia zaidi ya 100 ya mpunga.
Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Namtumbo Adeni Nchimbi ameahidi kutekeleza yote yaliyoagizwa na Kamati ya Siasa ya CCM Mkoa ili kumaliza migogoro baina na serikali na wananchi wanaozunguka hifadhi hizo.
Mmoja wa wananchi wa kijiji cha Mchomoro Said Huseni akizungumza baada ya maelekezo ya Kamati kwa niaba ya wananchi wenzake,amekishukuru Chama na serikali kuridhia kufanyika mapitio katika hifadhi hizo hali ambayo itaondoa migogoro baina ya serikali na wananchi ambayo imedumu kwa miaka mingi.
Amesema idadi ya wananchi katika vijiji vinavyozunguka hifadhi imeongezeka,ametolea mfano katika kijiji cha Mchomoro wakati yanafanyika makubaliano ya kwanza,kijiji kilikuwa na watu 6,000 ambapo hivi sasa idadi ya watu inakaribia 30,000 hivyo kuna changamoto ya ardhi.
Imeandikwa na Albano Midelo
Afisa Habari Mkoa wa Ruvuma
Julai 4,2020
Namtumbo
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.