HALMASHAURI ya Madaba wilayani Songea mkoani Ruvuma imetumia zaidi ya shilingi milioni 84 kutekeleza miradi ya ujenzi wa miundombinu ya madarasa katika shule za msingi Kiblang’ombe na Sokoine.
Hayo yamelezwa wakati Halmashauri hiyo inatoa taarifa kwa Kamati ya Siasa ya CCM Mkoa wa Ruvuma ya utekelezaji wa Ilani ya CCM wakati wa kutembelea na kukagua miradi ya maendeleo ya Halmashauri hiyo.
Akitoa taarifa ujenzi wa madarasa matatu katika shule ya msingi Kiblang’ombe ,Mwalimu Mkuu wa shule hiyo Marco Mkandawile amesema shule hiyo ilipokea shilingi milioni 60 kutoka Mamlaka ya Elimu Tanzania kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo na nguvu za wananchi ni zaidi ya milioni tano.
“Baada ya mradi kukamilika zimebaki sh. Milioni tatu, shule sasa imekuwa na vyumba vya madarasa vya kutosheleza na kuondoa msongamano wa wanafunzi madarasani,walimu na wanafunzi wana mazingira bora ya kufundishia na kujifunzia’’,alisisitiza Mkandawile.
Naye Mwalimu Mkuu wa shule ya msingi Sokoine Swalehe Mapondela amesema shule hiyo imetekeleza mradi wa ujenzi wa madarasa mawili kwa kiasi cha shilingi milioni 24.7 zilizotolewa na serikali na kwamba mradi umetekelezwa kwa mtindo wa force akaunti.
Mapondela amesema hali ya mradi wa madarasa hayo upo katika hatua za umaliziaji ukiwa umefikia asilimia 98 na kwamba kuchelewa kukamilika kwa mradi kumetokana na kuchelewa kwa fedha za mradi kutokana na fedha kuchelewa kuwekewa vifungu vya matumizi.
Hata hivyo amesema mradi unatarajia kukamilika mwishoni mwa mwezi Julai mwaka huu ambapo ameishukuru serikali kwa kuwezesha fedha za kutekeleza mradi huo ambao umewezesha wanafunzi kusoma kwenye mazingira rafiki.
Akizungumza mara baada ya kukagua miradi ya shule hizo,Mwenyekiti wa Kamati ya Siasa ya CCM Mkoa wa Ruvuma Odo Mwisho amezipongeza shule hizo kwa kutekeleza mradi huo na kubakiza fedha ambapo amelitaja lengo la serikali ni kuhakikisha maendeleo yanawafikia wananchi kwa kutekeleza miradi kwa asilimia 100.
Amesema fedha zinazotolewa na serikali zimetokana na walipa kodi hivyo zinatakiwa kusimamiwa na kutumika vizuri ili miradi inayotekelezwa ilingane na thamani ya fedha zinazotolewa na serikali.
Imeandikwa na Albano Midelo
Afisa Habari Mkoa wa Ruvuma
Julai 5,2020
Madaba
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.