KAMATI ya Siasa ya CCM Mkoa wa Ruvuma imetoa wiki moja kwa TANESCO kuhakikisha wanapeleka umeme kwenye mradi wa maji Madaba wilayani Songea ili wananchi waanze kunufaika na maji safi na salama.
Akizungumza baada ya kamati hiyo kukagua mradi wa maji Madaba ambao serikali imetoa zaidi ya shilingi bilioni mbili kutekeleza mradi huo,Mwenyekiti wa Kamati hiyo Oddo Mwisho amesema mradi huo umechukua muda mrefu ambapo hivi sasa serikali imedhamiria wananchi wa Madaba kupata maji na salama.
“Nampongeza Meneja wa RUWASA Mkoa wa Ruvuma ambaye ndani ya muda mfupi amesimamia miradi mingi ya maji iliyosababisha Mkoa wa Ruvuma kupata tuzo ya umahiri wa kusimamia miradi ya maji’’,alisema Mwisho.
Kwa niaba ya Kamati, Mwisho amewaagiza TANESCO Ruvuma kuhakikisha wanashughulikia umeme ili kuanzia wiki ijayo wananchi wa Madaba waanze kupata maji na kwamba Kamati ya Siasa haihitaji ubabaishaji katika kushughulikia suala ya kero ya maji kwa wananchi.
Kwa upande wake Mjumbe wa Kamati hiyo ambaye pia ni Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Christina Mndeme ameutaja mradi wa maji Madaba kuwa ni wa zamani na kwamba wananchi wamepata shida kwa muda mrefu.
Hata hivyo amesema RUWASA Mkoa wa Ruvuma wamefanya kazi kubwa ya kutekeleza mradi huo ambao upo katika hatua za mwisho kukamilika kwa asilimia 100.
Hata hivyo Mndeme amesema TANESCO wamechangia kuchelewesha mradi huo ambapo ametoa siku tano kuhakikisha wanamaliza kazi ya kupeleka umeme kwenye mradi huo na pasiwepo na kisingizio chochote.
“Wananchi wa Madaba hivi sasa wanahitaji maji,mimi nitapita hapa Alhamis,nikifika TANESCO hamjafanyakazi nitawaweka ndani wote,nataka tumalize huu mradi,TANESCO mkinizingua,tutazinguana,kila mtu avae sura ya kazi’’,alisisitiza Mndeme.
Awali Meneja wa RUWASA Wilaya ya Songea Mathias Charles amesema mradi huo hadi sasa umefikia zaidi ya asilimia 90 ambapo amezitaja kazi zilizokamilika kwa asilimia 100 ni ujenzi wa tanki la juu la kuhifadhia maji kwenye kijiji cha Lituta lenye ujazo wa lita 50,000.
Kazi nyingine zilizokamilika ni ujenzi wa tanki la kuhifadhia maji katika kijiji cha Kipingo lenye ujazo wa lita 100,000 na kwamba ujenzi wa vituo 21 kati ya 40 vya kuchotea maji vimekamilika na ununuzi wa vifaa mbalimbali vya ujenzi umekamilika kwa asilimia 98.
Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Olaph Pilly kwa niaba ya wananchi wa Madaba ameipongeza serikali kwa kutekeleza mradi huo wa maji ambao utaifanya kero ya maji Madaba kubakia historia.
Imeandikwa na Albano Midelo
Afisa Habari Mkoa wa Ruvuma
Aprili 19,2021
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.