ZAHANATI ya kijiji cha Njenga kata ya Mchoteka Halmashauri ya wilaya Tunduru mkoani Ruvuma,imepokea msaada wa vifaa mbalimbali kutoka kwa Kanisa la Upendo wa Kristo Masihi vitakavyosaidia utoaji wa huduma bora kwa wananchi.
Vifaa vilivyotolewa na kanisa hilo ni vitanda vya kulala watu wazima,vitanda vya kujifungulia vitanda kwa watoto wadogo na viti vya magurudumu manne(wheel chairs) kwa wagonjwa wanaohitaji msaada wa mtu mwingine ili kuwafikia watoa huduma.
Akipokea vifaa hivyo,muuguzi wa zahanati ya Njema Upendo Bora,amelishukuru Kanisa hilo kwa msaada huo kwani vifaa hivyo vitakwenda kuchochea uwajibikaji kwa watumishi na kutoa huduma bora kwa wagonjwa wanaofika kupata huduma za afya.
Alisema,vifaa hivyo vimetolewa kwa muda muafaka kwani kumekuwa na ongezeko kubwa la watu wanaofika katika kijiji hicho kwa ajili ya shughuli mbalimbali wakiwemo wanunuzi wa mazao na wafugaji ambao watahitaji kupata matibabu.
Mwenyekiti wa Serikali ya kijiji cha Njenga John Mtanga alisema,msaada wa vifaa tiba vilivyotolewa na kanisa hilo vitapunguza kero ya mama wajawazito wanaosubiri kujifungua au waliojifungua kulala zaidi ya mtu mmoja katika kitanda kimoja.
Kwa upande wake Askofu wa Kanisa la Upendo wa Kristo Masihi Noel Mbawala alisema,kanisa kupitia taasisi yake ya Kiuma imelazimika kutoa vifaa hivyo ili vitumike kuimarisha afya za watu kwa kutambua kuwa ili watu waweze kumjua Mungu na kushiri kwenye shughuli za maendeleo ni lazima wawe na afya njema.
Aidha alisema,kanisa limetoa vifaa tiba katika zahanati hiyo kutokana na mahitaji makubwa ya vifaa kwa ajili ya wagonjwa na kuunga mkono jitihada zinazofanywa na Serikali ya awamu ya sita za kuimarisha na kuboresha huduma za afya katika wilaya ya Tunduru.
Askofu Mbawala,ameipongeza serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa jithada zake katika kuimarisha huduma za afya,maji,umeme na miundombinu ya Barabara ambayo imewezesha kuboresha na kuimarisha maisha ya Watanzania.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.