SHULE ya sekondari ya Kigonsera iliyopo wilayani Mbinga mkoani Ruvuma ina historia ya kipekee hapa nchini kwa sababu ndiyo sekondari iliyoweza kuwatoa viongozi wawili wa ngazi ya juu kabisa nchini.
Ponsiano Ngungulu ni Mkuu wa sekondari ya Kigonsera anasema shule hiyo ilianzishwa mwaka 1938 ikiwa ni seminari ya kanisa katoliki chini ya Shrika la Wabenedikitini(Benedictine fathers) wa Peramiho hadi mwaka 1961 ilipochukuliwa na serikali.
Ngungulu anasema shule hiyo ya wavulana pekee, ina uwezo wa kuwahudumia wanafunzi 280 na kwamba tangu kuanzishwa kwake hadi sasa,shule hiyo imeweza kutoa jumla ya wahitimu 13,266.
“Shule wakati inaanzishwa na wakoloni ilikuwa na lengo la kutoa elimu ya dini ya kikristo hususani dhehebu la kanisa katoliki hivyo baada ya uhuru serikali iliamua kuitaifish ili iweze kuwahudumia watanzania wote bila ubaguzi wa kidini’’,anasema.
Hata hivyo anasema tangu mwaka 1961 hadi mwaka 2011 sekondari ya Kigonsera imekuwa inatoa elimu ya sekondari kwa wanafunzi wa kidato cha kwanza hadi cha nne na kuanzia mwaka 1998 hadi sasa sekondari hiyo imekuwa inatoa elimu ya kidato cha sita.
Sekondari ya Kigonsera imepata umaarufu mkubwa hapa nchini kwa sababu imeweka historia iliyotukuka baada ya viongozi maarufu wa kitaifa kusoma katika sekondari hiyo.
Mkuu wa sekondari ya Kigonsera anamtaja mmoja wa viongozi hao kuwa ni Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Benjamin Mkapa ambaye alisoma Kigonsera toka mwaka 1952 hadi 1953 kisha alihamia Ndanda mkoani Mtwara.
Ngungulu anamtaja Kiongozi mwingine wa kitaifa ambaye amesoma Kigonsera ni Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa ambaye alianza kidato cha kwanza na kuhitimu kidato cha nne katika sekondari hiyo mwaka 1980.
Licha ya viongozi hao sekondari ya Kigonsera imetoa viongozi wengine wengi hapa nchini ,miongoni mwao ni Dkt Modestus Kipilimba ambaye ni Balozi wa Tanzania nchini Msumbiji,Profesa Simon Mbilinyi aliyewahi kuwa Waziri wa Fedha na Mbunge wa Peramiho na Juma Homera Mkuu wa Mkoa wa Katavi.
Viongozi wengine waliosoma Kigonsera ni Katibu Mkuu Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Dkt Frolens Turuka,Hayati Askofu Mstaafu wa Jimbo la Mbinga Imanuel Mapunda,Hayati Askofu Mstaafu wa Jimbo la Njombe Raymund Mwanyika ,Askofu Mkuu Mstaafu wa Jimbo Kuu la Songea Norbeth Mtega,Askofu wa Jimbo la Lindi Mhashamu Bruno Ngonyani ,Askofu wa Jimbo la Mtwara Mhashamu Gabriel Mmole na Askofu wa Jimbo la Njombe Mhashamu Alfred Maluma .
Moto wa shule ya sekondari ya Kigonsera, Elimu ni ukombozi na dira ya shule ni kutoa elimu bora ya kupambana na changamoto mbalimbali zinazotokana na mabadiliko ya Dunia.
Imeandikwa na Albano Midelo
Afisa Habari wa Mkoa wa Ruvuma
Julai 10,2020
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.