KITUO cha Afya Mkasale Kata ya Namasakata Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma kimeanza kutoa huduma za upasuaji ambapo hadi sasa watu 51 wamefanikiwa kufanyiwa upasuaji.
Akitoa taarifa ya kituo hicho kwa Kamati ya Siasa ya CCM Mkoa wa Ruvuma,Mganga Mkuu wa kituo hicho Dr.Joseph Morris amesema kati ya watu waliofanyiwa upasuaji akinamama wajawazito ni 32 na wengine wasiokuwa wajawazito 19 na kwamba upasuaji kwa wote umefanyika kwa mafanikio makubwa.
Dr.Morisi amesema huduma ya upasuaji imeanza kutolewa katika kituo hicho tangu Machi mwaka huu ambapo idadi ya wagonjwa wanaohitaji huduma imekuwa inaongezeka na kwamba kituo kina uwezo wa kulaza wagonjwa 36 ambapo kwa siku wanapokea wagonjwa 60.
Amesema kituo hicho kinazungukwa na zahanati nane ambazo zinakitegemea kituo hicho katika huduma mbalimbali za afya na kwamba kituo pia kinahudumia watu kutoka tarafa ya Nakapanya na Tunduru mjini.
“Kituo hiki kilianzishwa mwaka 1989,ukarabati umefanyika kuanzia mwaka 2018 baada ya serikali kutoa kiasi cha shilingi milioni 400 na kazi ya upasuaji imeanza mwaka huu kwa ufanisi mkubwa’’.alisisitiza.
Naye Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Ruvuma Odo Mwisho amesema serikali ya CCM imefanyakazi kubwa ya kuwaondolea kero wananchi wa Kata ya Namasakata baada ya kuanza kutoa huduma za upasuaji katika kituo hicho cha afya.
‘’Hakuna aliyetegemea kituo hiki cha afya kingeweza kutoa huduma za upasuaji na wagonjwa wote waliofanyiwa upasuaji wametoka salama ,haya ni mafanikio makubwa sana,kwa sababu kabla ya kuwepo kituo hiki wazazi wengi wamepoteza maisha kwa kusafiri umbali mrefu kutafuta huduma’’,alisisitiza Mwisho.
Wananchi wa kijiji cha Mkasale wameishukuru serikali kwa kufanikisha ujenzi wa kituo hicho ambacho wamesema kimekuwa mkombozi kwa wananchi wote na kupunguza vifo ambavyo vilikuwa vinatokea kwa kukosa huduma jirani.
Kituo cha afya Mkasale baada ya kiufanyiwa ukarabati kinatoa huduma za wagonjwa wa nje,maabara,upasuaji,wodi ya wanaume,wodi ya wanawake,jengo la mama na mtoto na chumba cha kuhifadhia maiti.
Imeandikwa na Albano Midelo
Afisa Habari Mkoa wa Ruvuma
Julai 2,2020
Tunduru
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.