KIWANDA cha Wakulima wa zao la kahawa wilaya ya Mbinga(MCCCO),katika msimu wa mwaka 2022/2023 kimepokea na kukoboa zaidi ya tani 18,875 za kahawa kavu kutoka kwa vyama vya msingi vya Ushirika(Amcos).
Meneja Mkuu wa Kiwanda hicho Festo Chang’a alisema hayo ,wakati akizungumza ofisini kwake mjini Mbinga, kuhusiana na mafanikio ya kiwanda hicho chenye mchango mkubwa kiuchumi kwa wakulima na wilaya ya Mbinga.
Chang’a alisema,kiasi hicho ni kidogo ikilinganisha na uwezo wake wa kukoboa zaidi ya tani 35,000 kwa mwaka na hali hiyo imetokana na baadhi ya wakulima kutotambua kwamba kiwanda hicho ni mali yao na wanapaswa kupeleka kahawa kwa wingi.
Alisema,kwa kuwa kiwanda hicho kinakabiliwa na ushindani kutoka kwenye viwanda vingine,ni wajibu wa wakulima kupitia Amcos zao kuhakikisha wanapeleka kahawa katika kiwanda chao ambacho wana hisa nacho ili kuongeza mapato ya ushirika.
Aidha alisema,wanapopeleka kahawa wakulima watapata fursa zinazotolewa katika kiwanda hicho ikiwemo kuongeza nguvu wakati wa kuhudumia mashamba ya zao hilo ikiwa shambani ili kupata kahawa bora.
Chang’a alisema,kiwanda hicho ni muhimu kwani Kwa muda mrefu kinachangia shughuli za maendeleo katika vijiji mbalimbali ambavyo Amcos zao zinapeleka kahawa ikiwemo saruji,bati kwa ajili ya ujenzi wa shule,zahanati na miradi mingine ya maendeleo.
Alisema,kiwanda kinatoa ajira za muda na kudumu kwa baadhi ya wananchi wa Mbinga na wilaya ya jirani ya Nyasa na Songea ambapo vijana wa kike na kiume hupata ajira ambazo zinawawezesha kujipatia kipato kwa ajili ya familia zao.
Kwa mujibu wa Chang’a ni kuwa,kama Amcos hazipeleki kahawa kwa wingi katika kiwanda hicho basi husababisha kuwepo kwa upungufu mkubwa wa ajira hasa kwa akina mama ambao hawawezi kufanya kazi ngumu.
Hata hivyo alisema, katika msimu wa mwaka 2023/2024 wamejipanga kuhakikisha kiwanda hicho kikongwe wilayani Mbinga,kinapata kahawa nyingi kutoka kwa vyama vya msingi na vikundi mbalimbali vya wakulima vinavyojishughulisha na uzalishaji wa kahawa.
Afisa masoko wa kiwanda hicho David Haule alisema,kiwanda cha MCCCO kinasindika kahawa inayolimwa Mbinga ambayo ina ubora mkubwa na safi kwa matumizi ya kunywa na kuhamasisha wakulima na wananchi kunywa kahawa wanayolima wenyewe.
Haule alisema,sehemu kubwa ya kahawa inayosindikwa na kiwanda hicho usafirishwa nje ya mkoa wa Ruvuma kama vile Dar es slaam,Lindi,Mtwara,Dodoma,Iringa,Tanga na Mbeya kwa ajili ya kuuzwa.
Aliongeza kuwa,kahawa inayosindikwa katika kiwanda hicho imepata sifa kubwa kutokana na kuwa na radha nzuri na ndiyo inayopendwa zaidi Ulimwenguni kote ikilinganishwa na kahawa inayosindikwa katika viwanda vingine hapa nchini.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.