UTALII wa kiutamaduni bado ni nadharia changa katika nchi zinazoendelea ikiwemo Tanzania, kwa kuwa nchi hizo zimezoea kuona utalii wa ikolojia.
Utalii wa ikolojia ni kuona vitu vya asili kama kutembelea mbuga za wanyamapori, ndege, wadudu, milima, mabonde, misitu, maporomoko, mito, maziwa, mapango na chemchem.
Mkurugenzi wa Makumbusho ya Taifa ya Majimaji Balthazar Nyamusya anavitaja vivutio vya utalii wa kiutamaduni kuwa ni majengo ya makumbusho, historia, ngoma za asili, nyimbo za asili, lugha, michezo ya jadi, sanaa, vinyago, matamasha, vyakula, kilimo na mavazi.
Utalii wa kiutamaduni ni nadharia mpya hapa nchini ambapo serikali imeanza kuutambua utalii wa kiutamaduni na kuupa nguvu kubwa aina hiyo ya utalii ambayo inaweza kuleta mabadiliko makubwa katika sekta ya utalii hapa nchini.
Mkoa wa Ruvuma ni miongoni mwa mikoa michache nchini yenye fursa lukuki za utalii wa kiutamaduni na utalii wa ikolojia ambazo hadi sasa wananchi wamefaidika kwa kiwango kidogo kutokana na sekta hiyo kutopewa kipaumbele katika mkoa huo.
Ili kuhakikisha utalii wa kiutamaduni unachochea maendeleo, serikali ya Awamu ya Sita imeamua kuanzisha tamasha la kitaifa la utamaduni ambalo mwaka huu linafanyika mkoani Ruvuma kuanzia Julai 20 hadi 27 mwaka huu.
Tamasha la kitaifa la utamaduni lilianzishwa mwaka 2022 ikiwa ni kutekeleza kwa vitendo maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan aliyoyatoa alipokuwa mgeni rasmi mkoani Mwanza Septemba 8,2021 katika Tamasha la utamaduni la Bulabo.
Rais Samia aliagiza matamasha ya utamaduni kufanyika kwa mzunguko kila Mkoa ili watanzania wajue mila na desturi za kila Mkoa ambapo aliagiza kuwe na mashindano ya ngoma za asili na washindi wapewe Tuzo.
Malengo makuu ya tamasha la kitaifa la utamaduni ni kurithisha amali za utamaduni kwa vitendo, kuchochea maendeleo ya utalii wa kiutamaduni, Sanaa za asili,sekta za ubunifu wa asili, kuhamasisha utaifa,uzalendo na urithishaji wa maadili kwa mtanzania
Vivutio vya utalii wa kiutamaduni vilivyopo katika Mkoa wa Ruvuma ni majengo ya kihistoria, makanisa, makumbusho ya vita vya Majimaji, historia ya machifu, jiwe la Mbuji, mapango ya wamatengo na pango la mlima Chandamali lililokuwa maficho ya chifu Songea Mbano wakati wa vita ya Majimaji.
Siku za nyuma vivutio vya utalii wa kiutamduni kama vile majengo ya kale,maeneo ya kihistoria na makumbusho hayakupewa mtazamo wa kiuchumi zaidi.Mhadhili Msaidizi kutoka Idara ya Utalii wa Kiutamaduni Frank Kimaro anasema Maeneo hayo yalipewa mtazamo wa kielimu zaidi na kuundwa Idara za Mambo ya Kale na Idara ya Makumbusho ya Taifa.
Mabadiliko duniani ndiyo yaliyosukuma kuwepo kwa utalii wa kiutamaduni na nchi zilianza kutoa kipaumbele katika utalii wa kiutamaduni ndiyo maana hapa nchini Idara za Mambo ya kale na Makumbusho zilihamishwa kutoka Wizara ya Elimu na kuingia katika Wizara ya Utalii na Maliasili.
Mabadiliko ya utalii wa kiutamaduni hayawezi kuonekana kwa haraka badala yake inatakiwa watalaamu kuwahamasisha wananchi kutambua fursa zilizopo katika aina hiyo ya utalii na kuzitumia ipasavyo fursa zilizopo ili kujiletea maendeleo yao binafsi na Taifa kwa ujumla wake.
Ni vigumu kutenganisha utalii wa ikolojia na utalii wa kiutamduni kutokana na aina hizo mbili za utalii kuwa na mahusiano ya karibu,Watalii wanapoingia nchini wote wanavutika na utalii wa aina zote mbili.
Mtalii anapokwenda kutembelea utalii wa ikolojia kama mbuga za wanyama pia anaweza kupita katika maeneo yenye utalii wa kiutamaduni na kwamba fursa ya utalii wa kiutamaduni ni kubwa kwa wananchi wa kawaida kuliko aina nyingine za utalii.
Utalii wa kiutamaduni unazungumzia jamii husika na kwamba jamii hiyo inaweza kufaidika kutokana na utalii wa kiutamaduni ambao unapatikana katika eneo husika hadi kufikia ngazi ya kitaifa.
Unaweza kuona aina hii ya utalii ni tofauti na utalii wa ikolojia ambao tunaangalia zaidi mbuga za wanyama na maeneo ya asili ambayo yametengwa na serikali ambapo wahusika wakubwa ni serikali yenyewe na siyo watu binafsi, katika utalii wa kiutamaduni wahusika wakuu ni wananchi wenyewe .
Wananchi katika utalii wa utamaduni wanaweza kunufaika kuanzia kiwango cha familia, mtaa, kitongoji, kijiji, Wilaya, Mkoa na Taifa kwa hiyo utalii wa kiutamaduni unatoa fursa kubwa ya ukuaji wa uchumi kuanzia kwa mtu binafsi hadi kwa taifa.
Hata hivyo inaelezwa kuwa licha ya utalii wa utamaduni kuonekana kumlenga zaidi mwananchi wa kawaida, lakini kipato anachopata mwananchi huyo kwa kucheza ngoma au kuuza bidhaa za jadi na kazi nyingine za mikono kipato chake kimekuwa cha chini na kuwakatisha tamaa.
Vitu anavyovifanya mwananchi katika utalii wa kiutamaduni vina thamani kubwa kuliko mapato anayopata na kwamba katika hali ya kawaida vitu vya utamaduni vina thamani kubwa na vikiachwa kupotea haviwezi kupatikana tena kwa kuwa hakuna kiwango cha malipo kamili kwa shughuli za utalii wa kiutamaduni.
Bidhaa zinazotokana na utalii wa kiutamaduni kama samani zilizotengenezwa kwa miti na sanamu za kuchonga zimekuwa zinauzwa na watu binafsi kwa watalii na wageni wengine kwa bei za juu.
Nafasi ya utalii wa kiutamaduni ni kubwa katika kukuza uchumi wa nchi, utalii unachangia uchumi wa Tanzania katika kiwango kikubwa na kuchukua nafasi ya pili hivyo utalii endelevu una nafasi kubwa katika kuleta maendeleo endelevu.
Kuna nchi nyingi ambazo zimekuza uchumi wake kwa haraka kupitia utalii wa kiutamaduni zikiwemo Australia, Ujerumani, Uingereza na nchi nyingine za ulaya ambazo kutokana na ukosefu wa mbuga za wanyama wengi kama zilivyo katika Afrika wameamua kuendeleza utalii wa kiutamaduni zaidi kuliko utalii wa asili na kupata maendeleo makubwa kupitia aina hiyo ya utalii.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.