MSIMAMIZI wa Uchaguzi wa Jimbo la Peramiho Simon Bulenganija ametoa onyo kwa mawakala wa vyama vya siasa waliokusudia kuvuruga Uchaguzi Mkuu mkono wa sheria hautawaacha salama.
Bulenganija ametoa onyo hilo kwa nyakati tofauti wakati akiwaapisha kiapo cha kutunza siri mawakala wa vyama vya siasa ambao wameteuliwa na vyama vyao katika Mji mdogo wa Peramiho na Kijiji cha Mpitimbi katika Jimbo la Peramiho Mkoani Ruvuma.
Amesema kwa wakala yeyoto atakayejitoa ufahamu kwa lengo la kuvuruga Uchaguzi Mkuu, Oktoba 28, 2020 iwe,wakati wa kupiga kura, kuhesabu kura,kujumlisha kura na kutangaza matokea mkono wa sheria hauta muacha salama kwa sababu zoezi la uchaguzi lipo kwa mujibu wa kanuni taratibu na sheria za Nchi.
“Lazima mpime vizuri kazi ya kusimamia maslahi ya chama lakini pia umuhimu na ulazima wa kuzingatia sheria,kanuni,taratibu na maelekezo ya Tume”,alisema Bulenganija.
Ametahadharisha kila wakala kutimiza jukumu alilopangiwa na kuacha kuingilia jukumu ambalo wakala hakupangiwa katika kipindi cha kupiga kura,kuhesabu kura kujumlisha kura na kutangaza matokeo.
Hata hivyo amesema vyama ambavyo havijawasilisha orodha ya majina ya mawakala wa vyama vyao katika Ofisi ya Msimamizi wa jimbo la Uchaguzi hawataruhiswa kusimamia uchaguzi kwa mujibu wa maelekezo ya Tume ya Uchaguzi.
Amesema katika jimbo hilo vyama viwili tu ambavyo vimetimiza sharti hilo ambavyo ni Chama cha Maendeleo na Demokrasia (CHADEMA) na Chama cha Mapinduzi (CCM).
Amewakumbusha wananchi wote wenye sifa na vigezo kujitokeza kwa wingi kwenda katika vituo walivyojiandikisha kwenda kupiga kura siku ya Jumatano Oktoba 28,2020 ili ktimiza haki yao ya kikatiba ya kuhakikisha kila mtu anapiga kura kwa uhuru.
Amesema maandalizi yote ya zoezi la uchaguzi yanaenda vizuri na tayari Tume ya Taifa ya Uchaguzi imeshafikisha vifaa kwa asilimia 98 ambavyo vinatakiwa katika kufanikisha zoezi hilo.
Kwa upande wake Msimamizi Msaidizi wa Jimbo la Uchaguzi la Peramiho Kangese Masanja amesema mawakala ni kundi la watu muhimu katika kufanikisha zoezi la uchaguzi ,hivyo ni vema wakazingatia maelekezo yote yanayotolewa na Tume na kujiepusha na udanganyifu wawapo katika vituo vya kupigia kura.
Jimbo la Peramiho lina Kata 16,Vijiji 56,vituo vya kupigia kura 252 na jumla ya mawakala 509 waliapa kiapo cha kutunza siri katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.
Imeandikwa na Albano Midelo
Afisa Habari Mkoa wa Ruvuma
Oktoba 23,2020
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.