MAAFISA Elimu Watu Wazima katika Halmashauri zote mkoani Ruvuma wameagizwa kuhakikisha wanasimamia uwepo wa madarasa ya kisomo na SEQUIP katika kila Kata.
Agizo hilo limetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Ahmed Abbas Ahmed katika hotuba iliyosoma kwa niaba yake na Katibu Tawala wa Mkoa wa Ruvuma Mary Makondo katika kilele cha maadhimisho ya Juma la Elimu kimkoa ambayo yamefanyika Mbambabay wilayani Nyasa.
“Niwaombe wananchi kujiunga kwa wingi katika madarasa hayo kama ilivyo dhamira ya Rais wetu Dkt.Samia Suluhu Hassan kuhakikisha kila kijana wa kike aliyekatisha masomo anarejeshwa shuleni’’,alisisitiza Kanali Abbas.
Kupitia maadhimisho hayo,Mkuu wa Mkoa amewaagiza wakurugenzi wote wa Halmashauri na maafisa Elimu Msingi na Sekondari wahakikishe kuwa elimu ya watu wazima inatiliwa mkazo kwa kuweka mikakati mizuri ili iweze kutekelezwa kikamilifu.
Akitoa taarifa ya utekelezaji wa shughuli za elimu ya watu wazima na elimu nje ya mfumo rasmi kwenye maadhimisho hayo,Afisa elimu Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Mwl.Mathias Tilia amesema Mkoa kwa kushirikiana na Taasisi ya elimu Tanzania unatekeleza program kwa wasichana waliokatisha masomo ya sekondari ambapo hadi sasa jumla ya wanafunzi 228 wananufaika na mradi huo.
Tilia amesema Mkoa wa Ruvuma una jumla ya vituo 70 vya elimu ya msingi kwa Watoto walioikosa (MEMKWA) vyenye jumla ya wanafunzi 317 kati yao wavulana 231 na wasichana 186 na kwamba wanafunzi hao walikosa fursa ya kupata elimu katika mfumo rasmi kutokana na changamoto mbalimbali za kimaisha.
Ameongeza kuwa Mkoa wa Ruvuma una vituo vitano vya ufundi stadi ambavyo hutoa mafunzo kwa wanafunzi waliomaliza elimu ya msingi na sekondari katika fani za useremala,ushoni,udobi na upishi na kwamba vituo hivyo vinawapa ujuzi wa stadi mbalimbali vijana ili kuwawezesha kukabiliana na changamoto za kimaisha.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Nyasa Mheshimiwa Peres Magiri akizungumza kwenye maadhimisho hayo yenye kaulimbiu ya ujumuishi katika elimu bila ukomo kwa ujuzi,ustahimilivu,amani na maendeleo,amesisitiza wananchi kuendelea kupata elimu kupitia mfumo usiokuwa rasmi kwa kuwa elimu haina mwisho.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.