Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Christina Mndeme amekabidhi Pikipiki 20 kwa maafisa Tarafa wa Mkoa wa Ruvuma ikiwa ni utekelezaji wa ahadi ya Rais Dkt.John Magufuli aliyoitoa Ikulu mwaka 2019 katika kikao cha maafisa tarafa wote nchini..
Akizungumza kabla ya kukabidhi pikipiki hizo, Mndeme amemshukuru Rais kwa upendo ambao haujawahi kutokea tangu nchi yetu ipate Uhuru kwa kiongozi wa juu wa Taifa kukaa kikao Ikulu na maafisa Tarafa wote nchini.
Amelitaja lengo la kutoa pikipiki hizo ni kuhakikisha shughuli za maendeleo kwa maafisa tarafa zinafanyika kwa viwango vinavyotakiwa na kuona uchumi wa wananchi unaimarishwa ipaswavyo.
Amesema pikipiki hizo zinagawanywa katika wilaya zote tano za Mkoa wa Ruvuma ambapo wilaya songea imepata pikipiki nne, Mbinga tano,Nyasa mbili,Tunduru saba na Namtumbo mbili.
“Pikipiki hizi mnapewa kusaidia katika kurahisisha mawasiliano kati ya ngazi ya kata na Halmashauri kwa upande mmoja na Serikali Kuu na Serikali za Mitaa kwa upande mwingine,pikipiki hizi zitunzwe ili ziweze kudumu kwa muda mrefu’’,alisisitiza Mndeme.
Amewaagiza Maafisa Tarafa wafuatilie na kusimamia utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika maeneo yao na kuhakikisha wanasimamia ulinzi na usalama katika kata zilizomo ndani ya Tarafa husika.
Kwa upande wake Katibu Tawala wa Mkoa wa Ruvuma Steven Ndaki amesema pikipiki hizo zilizotolewa na Rais Dkt.John Magufuli ni utekelezaji wa ahadi yake aliyoitoa kwa maafisa hao walipokuwa Ikulu mjini Dar es salaam.
Akizungumza kwa niaba ya maafisa tarafa waliopata pikipiki hizo,Afisa Tarafa wa Songea mjini Mashariki Agustino Chazua amempongeza Rais Dkt.John Magufuli kwa kutekeleza ahadi yake kwa maafisa tarafa.
Amesema hivi sasa pikipiki hizo zitawasadia kutekeleza majukumu yao kwa asilimia 100 ambapo watahakikisha wanakwenda kusikiliza kero mbalimbali kwa wananchi katika vijiji vyote .
Imeandaliwa na Albano Midelo
Afisa Habari Mkoa wa Ruvuma
Mei 11,2020
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.