MAAGIZO yote sita yaliyotolewa na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) Oktoba 2022 katika Halmashauri ya Madaba wilayani Songea mkoani Ruvuma hayajatekelezwa hadi sasa.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Ahmed Abbas Ahmed katika hotuba yake iliyosomwa kwa niaba yake na Mkuu wa Wilaya ya Mbinga Mheshimiwa Kisale Makoli kwenye kikao cha kujadili utekelezaji wa maagizo ya Kamati ya LAAC kilichofanyika kwenye ukumbi wa Halmashauri ya Madaba.
Maagizo hayo ni Pamoja na Halmashauri kuweka mikakati ya kufanikisha ukusanyaji wa mapato ya ndani yasiyopungua sh.bilioni mbili,kulipa kodi ya zuio ya shilingi milioni 24.9 kwa TRA,kusimamia suala la fidia ya sh.milioni 229.8 inayotokana na kuvunjwa kwa mkataba na TBA,kukusanya sh.milioni 8.2 kutoka kwenye vikundi na kufunga mfumo wa GOT-HOMIS kwenye vituo vya kutolea huduma za afya.
Kanali Abbas amesema Kamati ya LAAC ilitoa maagizo hayo sita ambayo yalipaswa kutekelezwa kikamilifu na Menejimenti ya Halmashauri hiyo.
“Hali ya utekelezaji hadi sasa hairidhishi kabisa,hakuna agizo hata moja ambalo limetekelezwa na kufungwa,pia mwenendo wa kushughulikia hoja na mapendekezo ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali CAG bado hauridhishi kabisa’’,alisisitiza Kanali Abbas.
Kutokana na hali hiyo Mkuu wa Mkoa amewaomba waheshimiwa madiwani kufuatilia kwa karibu na kuhakikisha hoja zote zinajibiwa ipasavyo na kuweka mikakati ya kuhakikisha hoja hizo hazijirudii tena.
Kanali Abbas amewataka wakuu wa Idara kushiriki ipasavyo katika kuandaa majibu ya hoja na utekelezaji wa mapendekezo ya CAG ambapo ameuagiza uongozi wa Halmashauri hiyo kuchukua hatua mapema za kinidhamu kwa watumishi wanaozalisha hoja.
Katika Halmashauri hiyo hadi sasa kuna jumla ya hoja na mapendekezo 52 ambayo yanatakiwa kufanyiwa kazi ili yafungwe.
Awali Katibu Tawala wa Mkoa wa Ruvuma Rehema Madenge akizungumza kwenye kikao hicho ameuagiza uongozi wa Halmashauri hiyo kuhakikisha wanajitahidi kujibu hoja zote kwa wakati ,kwa usahihi na kushirikiana watendaji wote wa Halmashauri husika kujibu hoja.
Amesisitiza kuwa hoja hizo zinazalishwa na watumishi hivyo watumishi wenyewe wanatakiwa kujibu hoja zote kwa wakati kama ilivyoelekezwa ili Kwenda na muda uliopangwa.
Akizungumza kwa niaba ya waheshimiwa Madiwani,Naibu Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Mheshimiwa Oraph Pilly amesema wamesikitishwa na taarifa ya kushindwa kutekeleza kwa wakati maagizo yote sita ya LAAC katika Halmashauri hiyo.
Kutokana na hali hiyo waheshimiwa madiwani hao wamemwomba Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo ifikapo Aprili 5 mwaka huu kufanya kikao maalum cha kuangalia nini kilisababisha kushindwa kutekelezwa maagizo ya LAAC kwa wakati.
Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Mheshimiwa Teofanes Mlelwa ameridhia kufanyika kwa kikao hicho maalum ambapo amesisitiza kuwa amekosa amani kutokana na Halmashauri hiyo kushindwa kutekeleza maagizo hayo kwa wakati na kwamba amepokea maagizo yote yaliyotolewa na Mkuu wa Mkoa na kuahidi kuyafanyia kazi.
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma amefanya vikao vya kujadili utekelezaji wa maagizo ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa yaliyotolewa katika mwaka wa fedha wa 2021/2022 katika Halmashauri saba za Mkoa wa Ruvuma.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.