JUMLA ya shilingi milioni 196 zimetolewa na serikali kutekeleza miradi ya ujenzi katika shule ya Sekondari Mahanje iliyopo Halmashauri ya Madaba Wilaya ya Songea mkoani Ruvuma.
Afisa Elimu Sekondari wa Halmashauri hiyo Michael Hadu amesema kati ya fedha hizo shilingi milioni 150 zimetumika kwa kujenga mabweni mawili,milioni 40 zimejenga madarasa mawili na milioni 6.6 zimetumika kujenga matundu ya vyoo.
Amesema mabweni hayo yana uwezo wa kulaza wanafunzi 160 kila moja hivyo kupunguza kero kwa wanafunzi wa kike ambao walikuwa wanasafiri kila siku kilometa 24 kwenda na kurudi kwenye makazi yao.
Hata hivyo amesema Halmashauri ya Madaba ina jumla ya shule nane za sekondari ikiwemo shule ya sekondari Mahanje ambayo imefanikiwa kujengewa mabweni mawili ikiwa na wanafunzi zaidi ya 526 wanaosoma kidato cha kwanza hadi cha nne.
“Tuliweka mikakati ya kuboresha miundombinu ya shule hiyo ikiwemo mabweni,maabara,madarasa,maktaba na vyoo kwa kweli mabweni haya yamesaidia kupunguza mimba kwa wanafunzi na kuongeza ufaulu”,alisema Hadu.
Akizungumzia maendeleo ya taaluma katika Halmashauri hiyo,Hadu amesema kwa miaka miwili mfululizo 2019 na 2020,Halmashauri hiyo imeshika nafazi ya kwanza kimkoa kati ya Halmashauri nane za Mkoa wa Ruvuma katika mtihani wa Taifa wa kidato cha nne.
Kaimu Mkuu wa shule ya sekondari Mahanje Agastini Mikibalisi amesema ufaulu katika shule hiyo umeongozeka na kuondoa alama ya sifuri ambapo mwaka 2018 shule hiyo ilishika nafasi ya 25 kati ya shule 75 za Mkoa wa Ruvuma,mwaka 2019 ilishika nafasi ya 35 kati ya shule 137 za Mkoa wa Ruvuma na mwaka 2020 ilishika nafasi ya 24 kati ya shule 145 za Mkoa wa Ruvuma.
Amesema mabweni hayo yameleta faida katika shule hiyo na kufikia idadi kubwa ya wanafunzi wanaohudhuria masomo yao na kufanya vizuri katika mitihani yao.
Imeandikwa na Albano Midelo
Afisa Habari Mkoa wa Ruvuma
Machi 19,2021
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.