Na Albano Midelo,Songea
UZALISHAJI wa madini ya makaa ya mawe katika Mkoa wa Ruvuma umekuwa chanzo kikubwa cha mapato ya serikali ambapo katika mwaka wa fedha wa 2023/2024,serikali imeweza kuuza tani 1,356,249.84 za makaa ya mawe zenye thamani ya Dola za Marekani Zaidi ya milioni 144.9.
Kwa mujibu wa taarifa ya Afisa Madini Mkazi Mkoa wa Ruvuma,kiasi hicho cha madini kimeuzwa katika kipindi cha kuanzia Julai hadi Septemba 2023 pekee.
Kupitia mauzo hayo serikali imekusanya kiwango cha mrabaha wa Dola za Marekani 3,937,434.98 na ada ya ukaguzi Dola za Marekani 914,034.68 na kwamba madini hayo yameuzwa ndani ya nchi,nchi Jirani,barani Ulaya na Asia kupitia bandari ya Mtwara na Dar es salaam.
Hata hivyo Ofisi ya Afisa Madini Mkazi Mkoa wa Ruvuma katika kipindi cha mwaka wa fedha 2023/2024 ilipangiwa kukusanya jumla ya shilingi bilioni 41 na kwamba katika kipindi cha kuanzia Julai hadi Desemba ofisi hiyo ilikusanya Zaidi ya shilingi bilioni 13 sawa na asilimia 64.
Uchimbaji na uuzaji wa makaa ya mawe mkoani Ruvuma ulianza mwaka 2011 kukiwa na Kampuni moja ya uchimbaji ya Tancoal Energy ambapo hadi kufikia mwka 2019 wadau wengi walijitokeza na kufanya uwekezaji mkubwa katika uzalishaji wa madini ya makaa ya mawe.
Kwa mujibu wa taarifa ya Afisa Madini Mkazi,kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita,Mkoa wa Ruvuma umeweza kupata wawekezaji wengi katika uchimbaji,ununuzi na uchenjuaji madini ya makaa ya mawe.
Ameutaja mchango wa sekta ya madini mkoani Ruvuma kuwa ni Pamoja kutoa ajira kwa mtu mmoja mmoja na kupunguza utegemezi,kuongeza fedha za kigeni kutokana na mauzo ya madini nje ya nchi na kuongeza mapato ya Halmashauri yatokanayo na ushuru wa huduma.
Hata hivyo taarifa hiyo imezitaja changamoto za sekta ya madini mkoani Ruvuma kuwa ni Pamoja na uharibifu wa mazingira kutokana na kukata miti na kuchafua vyanzo vya maji,ubovu wa barabara ya kutoka migodini na changamoto ya upimaji wa viwango vya ubora wa madini ya makaa ya mawe.
Changamoto nyingine ni kukosekana kwa teknolojia ya kisasa ya kuongeza ubora wa makaa ya mawe ili kushindana na soko,uwepo wa leseni za utafiti na uchimbaji ambazo haziendelezwi,uelewa mdogo wa taarifa za kijiolojia,utambuzi wa aina za madini,thamani yake na masoko ya madini jambo linalosababisha kusimama kwa uzalishaji wa madini ya shaba katika eneo la Mbesa wilayani Tunduru.
Ameitaja Mikakati ya kukabiliana na changamoto hizo kuwa ni kuendelea kuhamasisha wachimbaji wa makaa ya mawe na wawekezaji wengine kuleta mitambo ya kuosha madini ili kuongeza ubora,kusimamia kurudishwa kwa shughuli mgodi wa Tancoal Energy na kuendelea kutoa elimuya sheria ya madini.
Ofisi ya Madini Mkoa wa Ruvuma pia inasimamia masoko mawili ya madini ya dhahabu na vito yaliyopo wilayani Songea na Tunduru.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.