Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Christina Mndeme amepokea msaada wa Vifaa vya kupambana na Corona vyenye thamani ya sh. milioni 1.5 kutoka Baraza la Makanisa ya Kipentekoste Tanzania (CPCT) Mkoa wa Ruvuma.
Hafla ya kukabidhi vifaa hivyo imefanyika leo katika viwanja vya ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma mjini Songea na kuwashirikisha viongozi mbalimbali wa CPCT.
Mndeme amelishukuru Baraza la CPCT Mkoa wa Ruvuma kwa msaada huo ambao amesema tangu Ugonjwa huo uingie mkoani Ruvuma,ni mara ya kwanza kupokea msaada kutoka kwenye madhehebu ya Dini.
Hata hivyo Mndeme amewaomba Viongozi wa Dini kuendelea kumuomba Mungu na Kumshukuru kwa Neema zake ili Taifa la Tanzania liendelee kuwa salama dhidi ya corona.
Mndeme amesema hadi kufikia Mei 4,mwaka huu katika Mkoa wa Ruvuma kwenye vituo nane vya kulaza wagonjwa wa corona, hakuna Mgonjwa hata mmoja na kwamba Mkoa upo salama ambapo ametoa rai kwa viongozi wa dini kuendelea kufanya maombi ili ugonjwa huo uweze kutokomezwa nchini na duniani kote.
‘’Mimi niendelee kuwaomba sana viongozi wa dini, kwa majitoleo yenu kwa watanzania, na kuliombea Taifa Letu na Rais wetu anaendelea kutuhimiza kuchukua Tahadhari,na mimi nachukua fursa hii kuwaahidi vifaa hivi vitatumika kwa malengo kusudiwa’’. Alisema
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Umoja wa Makanisa ya Kipentekoste Mkoa wa Ruvuma Mchungaji Andrew Kyando amevitaja vifaa ambavyo CPCT wamevitoa kuwa ni ndoo kumi za kunawia mikono na sabuni za maji 30.
Vifaa vingine ni mashine tano za kunawa maji ambazo zinatumika bila kugusa kwa ajili ya usalama zaidi,kipima joto la mwili kimoja(Thermal scanner) ambapo amesema vifaa vyote vimegharimu shilingi milioni 1.5.
Amesema CPTC inaunga mkono juhudi za serikali katika vita ya corona na kwamba inatambua umuhimu wa kutoa msaada huo ili wananchi wa Mkoa wa Ruvuma waendelee kujikinga na wawe salama dhidi ya maambukizi ya virusi vya corona.
Naye Katibu wa Baraza la CPCT Mchungaji Elimu Mwenzegule amemchukuru Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma kwa kuwashirikisha Maaskofu,Wachungaji tangu ulipoingia ugonjwa hatari wa Corona Nchini.
Mchungaji Mwenzegule amesema anamshukuru Mungu kwa kusikiliza maombi ya watanzania ambapo hivi sasa maambukizi ya corona nchini yamepungua kwa kiasi kikubwa.
Baraza la makanisa ya kipentekoste Tanzania linajumuisha umoja wa makanisa ya kilokole zaidi ya 80 yalipo nchini.
Imeandikwa na Albano Midelo
Afisa Habari wa Mkoa wa Ruvuma
Juni 4,2020
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.