MAMLAKA ya maji safi na usafi wa mazingira Mbinga mjini(Mbiuwasa),imefanikiwa kusambaza huduma ya maji safi na salama kwa wakazi wa mji wa Mbinga na maeneo ya pembezoni kwa asilimia 79.2.
Mkurugenzi Mtendaji wa Mbiuwasa Mhandisi Yonas Ndomba alisema hayo jana,wakati akieleza utekelezaji wa shughuli mbalimbali na mafanikio ya mamlaka hiyo katika kipindi cha miaka miwili ya uongozi wa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan.
Alisema kabla ya Rais Dkt Samia Hassan kuingia madarakani,Mbiuwasa ilikuwa na uwezo wa kusambaza huduma ya maji kwa asilimia 52.5 tu katika kata tano,lakini sasa eneo linalopata huduma ya maji safi na salama limeongezeka hadi kufikia kata 8.
Ameongeza kuwa,idadi ya wateja waliounganishiwa huduma ya maji safi na salama imeongezeka kutoka 2,900 mwaka 2021 hadi 4,332 kufikia mwezi Disemba mwaka 2023.
Ndomba alitaja mafanikio mengine ni kuongeza mtandao wa maji,kufunga dira(mita)kwa wateja wote,kuongeza ubora wa maji na kuwajengea uwezo watumishi wake ili waweze kutekeleza majukumu yao ipasavyo.
Kwa mujibu wa Ndomba,mafanikio hayo kwa Mbiuwasa yamepatikana baada ya serikali kupitia wizara ya maji kutoa zaidi ya shilingi bilioni 1.5 kwa mwaka wa fedha 2021/2022 zilizofanikisha kujenga mradi mkubwa wa maji wa Lusaka.
Alisema,kukamilika kwa mradi huo na mingine itakayotekelezwa katika maeneo mbalimbali,inalenga kuhakikisha huduma ya maji katika mji wa Mbinga inafika karibu na wananchi,kuchochea shughuli mbalimbali za maendeleo na kumtua mama ndoo kichwani.
Katika hatua nyingine Ndomba alisema,kwa mwaka wa fedha 2023/2024 wanatarajia kutekeleza mradi mkubwa wa maji utakao gharimu shilingi bilioni 4.6 fedha kutoka serikali kuu kwa ajili ya kuwezesha mji wa Mbinga kuwa na huduma ya maji safi na salama kwa asilimia 100.
Ndomba,amewaomba wakazi wa mji wa Mbinga kuanza kuingiza maji ndani ya nyumba zao
badala ya kutumia vituo maalum vya kuchotea maji(DPS) na kuwa walinzi wa miradi na miundombinu inayojengwa ili iweze kudumu kwa muda mrefu.
“sasa hivi tunaendelea na kampeni ya kuhamasisha wananchi kuhusiana na ujenzi wa vyoo bora ambavyo vinahitaji maji ya kutosha,kwa hiyo ni muhimu watu wavute maji kwenye nyumba zao”alisisitiza Ndomba.
Baadhi ya wakazi wa kata ya Betherehemu Halmashauri ya mji Mbinga,wamemshukuru Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha zilizofanikisha kujenga na kukamilika kwa mradi wa maji wa Lusaka.
Wamesema,mradi huo umepunguza shida ya upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama na kuwaondolea usumbufu wa kuamka usiku wa manane kwenda kutafuta maji kwa ajili ya matumizi ya familia zao.
Diwani wa kata ya Betherehemu Ngonepo Amanyisye alisema huduma ya maji safi na salama katika kata hiyo ilikuwa changamoto kubwa, lakini katika kipindi cha miaka miwili ya Serikali ya awamu ya sita kero hiyo imepungua kwa asilimia 85.
Alisema,hapo awali wananchi hasa wanawake wa kata ya Betherehemu ndiyo walikuwa waathirika wakubwa zaidi kwani walilazimika kuamka usiku wa manane kwenda kutafuta maji yaliyopatikana
kwenye visima vya asili na mabondeni licha ya maji hayo kutokuwa safi na salama hasa wakati wa masika.
Alisema,mradi wa maji Lusaka umeleta mapinduzi makubwa ndani ya kata ya Betherehemu kwani sasa hakuna mwananchi anayekwenda mtoni kuchota maji au kutumia maji ya visima vya asili kwa matumizi yao ya kila siku.
Hata hivyo,ameiomba serikali kupitia wizara ya maji kuendelea kutenga fedha za kutosha kwa ajili ya kusambaza mtandao wa maji katika maeneo mbalimbali ili wananchi wapate huduma hiyo karibu na makazi yao.
Laurent Ngonyani mkazi wa Majengo alisema, siku za nyuma hali ya huduma ya maji haikuwa nzuri ambapo wananchi waliamua kuchimba visima vifupi na virefu kwenye makazi yao ili angalau wapate maji kwa ajili ya matumizi yao.Ameishauri Mbiuwasa,kuhakikisha inasogeza bomba kuu kwenye makazi yao ili kuwapunguzia wananchi gharama kubwa ya kuingiza maji katika nyumba zao.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.